Peter Manyika kuagwa Mbezi na kuzikwa kesho Kinondoni

Kipa na Kocha wa zamani wa makipa wa Yanga na timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Peter Manyika anatarajiwa kuzikwa kesho, Jumatano, Januari 28, 2026 katika Makaburi ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Taarifa iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanasoka wa zamani Tanzania, Ibrahim Masoud ‘Maestro’ imeeleza kuwa shughuli zote za msiba mazishi ya Manyika zitaanzia nyumbani kwake Mbezi Marambamawili.

“Naomba nitoe taarifa. Mazishi ya ndugu yetu Nahodha wa zamani wa Taifa Star, Peter Manyika yatafanyika siku ya Jumatano saa kumi jioni katika Makaburi ya Kinondoni. Hivyo basi mwili wa marehemu utachuliwa Jumatano asubuhi katika Hospitali ya Mwananyamala na kuelekea nyumbani kwake Mbezi Marambamawili halafu baadaye kurejea Makaburi ya Kinondoni,” amesema Maestro.

Manyika ambaye hadi umauti unamkuta alikuwa Kocha wa Makipa wa namungo FC, aliaga dunia jana Jumatatu, katika Hospitali ya St. Monica Dar es Salaam alikopelekwa kupatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla.

Atakumbukwa kwa mchango mkubwa alioutoa akiwa mchezaji na kocha kwa timu mbalimbali alizozitumikia.

Mwaka 2003, Manyika aliiongoza Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kutwaa ubingwa wa mashindano ya Kombe la Chalenji yanayohusisha timu za taifa kutoka nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Mwaka 1999 aliiongoza Yanga kutwaa ubingwa mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na kabla ya hapo mwaka 1998 aliiongoza Yanga kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.