CCM MKOA WA DODOMA YAADHIMISHA KUZALIWA KWA DKT. SAMIA,YATOA WITO UTUNZAJI WA MAZINGIRA.

Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma kimeadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kukata keki na kupanda miti ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za utunzaji wa mazingira na kuhakikisha Jiji la Dodoma linaendelea kuwa la kijani.

Akizungumza mapema leo, Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbanga, amesema kuwa maadhimisho hayo yamelenga kuenzi mchango mkubwa wa Rais Samia katika kulinda, kutunza na kuhifadhi mazingira nchini, hususan katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema Dkt. Samia ni mwasisi wa harakati za upandaji miti nchini, akieleza kuwa akiwa Makamu wa Rais alizindua zoezi  la upandaji miti katika eneo la Makutupora mkoani Dodoma, jambo lililoweka msingi wa kampeni za utunzaji wa mazingira zinazoendelea kutekelezwa hadi sasa.

Mbanga ameongeza kuwa CCM Mkoa wa Dodoma imeona ni jambo la muhimu na la heshima kubwa kuadhimisha siku hiyo kwa kupanda miti, kama njia ya kuendeleza maono na mwelekeo wa Rais Samia katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Ameeleza kuwa upandaji na utunzaji wa miti ni jambo la msingi katika kuboresha mazingira, kusaidia upatikanaji wa mvua, kupunguza athari za joto pamoja na kuboresha mwonekano wa Jiji la Dodoma na maeneo yake ya jirani.

Amehitimisha kwa kuwataka wanachama wa CCM pamoja na wananchi wa Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kutunza mazingira kwa kupanda na kutunza miti, akisisitiza kuwa mazingira bora ni msingi wa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.