RC Batilda aiomba Hazina kuzibana taasisi zinazotoa mikopo ‘kausha damu’

 

Na MASHAKA MHANDO, TANGA.

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Buriani, ameiomba Wizara ya Fedha kuzibana taasisi za fedha zinazotoa mikopo kwa riba kandamizi, huku akitangaza kuanza rasmi kwa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote mkoani humo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Rais ndani ya siku 100 za uongozi wake.

Akifunga kilele cha Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa katika viwanja vya Usagara Jijini Tanga, Dkt. Batilda alitembelea banda la taasisi ya BRAC na kuelezea kusononeshwa na riba kubwa ya asilimia 3.5 kwa mwezi (wastani wa 40% kwa mwaka) wanayotozwa akina mama. 

“Wizara ya Fedha imewaelekeza wakae chini washushe riba hiyo walau ifike asilimia 1.5 ili kuwapunguzia adha akina mama. Tunataka mikopo iwakomboe, siyo iwakandamize,” alisema Dkt. Batilda.

Katika hatua nyingine, Dkt. Batilda amewatangazia wakazi wa Tanga kuanza kutolewa kwa vifurushi vya Bima ya Afya kwa Wote, jambo ambalo lilikuwa moja ya kipaumbele na ahadi kuu ya Rais ndani ya siku zake 100 za kwanza madarakani.

Alibainisha kuwa zoezi hilo sasa limeanza rasmi nchini kote, ambapo taasisi mbalimbali za bima ya afya zimeanza kutoa vifurushi hivyo vyenye gharama nafuu ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata matibabu bila kikwazo cha fedha.

Alizitaka taasisi za bima kutumia elimu ya fedha waliyoitoa wiki hii kuwahamasisha wananchi kujiunga na vifurushi hivyo sasa.

Mkuu wa Mkoa amezitaka benki za NMB, NBC, na Benki ya Mwalimu kubuni bidhaa zinazogusa wananchi wa chini na kuhakikisha jumuishi la fedha (Financial Inclusion) linafika hadi vijijini.

Dkt. Batilda amewasihi wananchi kutumia wasuluhishi wa migogoro ya fedha walioainishwa na serikali na kujiepusha na mikopo isiyo rasmi inayoweza kuwapotezea mali zao.

Awali akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Kaimu Kamishina wa Idara ya Uendeshaji wa taasisi ya fedha, Dionesia Mjema alibainisha kuwa tangu kuanza kwa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (2020/21 – 2029/30), Serikali imefanikiwa kutoa elimu kwa jumla ya Watanzania 64,125 katika mikoa 17 nchini.

“Katika idadi hiyo, tumefarijika kuona mwitikio wa wanawake ni mkubwa zaidi, ambapo jumla ya wanawake 41,680 wamefikiwa na elimu hii ikilinganishwa na wanaume 22,445. 

Hii inadhihirisha kuwa nguzo ya uchumi wa familia ambayo ni mwanamke, imeanza kuimarika kitaaluma,” alisema.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha kuanzia tarehe 19 hadi 26 Januari 2026, wananchi wa Tanga wamepata fursa ya kipekee ya kujifunza kupitia nyenzo maalum ya Wizara kuhusu usimamizi wa fedha binafsi, uwekezaji katika masoko ya mitaji (hatifungani), bima ya amana, na namna ya kuepuka mikopo yenye masharti kandamizi.

Maadhimisho hayo yaliyobeba kauli mbiu isemayo “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii”, yamehusisha taasisi kubwa za fedha nchini zikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), TIRA, CMSA, na wadhamini wakuu kama Benki ya NMB, NBC, Benki ya Biashara ya Mwalimu, UTT-AMIS, na PSSSF.

Akihitimisha alisema mafanikio yaliyopatikana Tanga yanatoa dira kwa Wizara kuendelea kuratibu maadhimisho hayo katika mikoa mingine kila mwaka, kwa lengo la kukuza Pato la Taifa na kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na nidhamu ya matumizi ya rasilimali fedha.

Nao baadhi ya wananchi walioshiriki, wakiwemo wavuvi na wajasiriamali wadogo (SMEs), wameishukuru Serikali kwa kuleta huduma hizo karibu, wakisema sasa wanaelewa umuhimu wa kukata bima za vyombo vyao na kuweka akiba kupitia mifuko ya uwekezaji wa pamoja.