Dili jipya la Dube, Wasaudia, Morocco wakitia timu Yanga

WAKATI mkataba wa mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube ukielekea ukingoni, mabosi wa klabu hiyo wameanza hesabu mapema za kuhakikisha staa huyo hachomoki Jangwani.

Dube aliyetua Yanga mwanzoni mwa msimu wa 2024-2025 akitokea Azam, alisaini mkataba wa miaka miwili kukitumikia kikosi hicho unaomalizika Juni 2026.

Mwanaspoti linafahamu kuwa, baada ya Dube kucheza michuano ya AFCON 2025 akiwa na Zimbabwe, huku akifunga bao moja wakati timu hiyo ikiishia makundi, ofa zimeanza kumiminika, huku nyingi zikitokea Saudi Arabia na Morocco.

Jambo hilo limeanza kuiwashia taa ya hatari Yanga, ambayo imesalia na mkataba wa miezi sita pekee na mchezaji huyo, huku sheria zikimpa nafasi Dube kuanza mazungumzo na klabu yoyote itakayohitaji huduma yake.

Taarifa kutoka Yanga zililiambia Mwanaspoti, klabu hiyo imeanza mazungumzo na Dube ili kuona uwezekano wa kumwongeza mkataba mapema kabla ya mwisho wa msimu kufika.

“Yanga inataka kukwepa presha ya mwisho wa msimu na mastaa wote wanaotaka kubaki nao watawaongeza mikataba mapema wakianza na Dube, ingawa ana ofa kubwa nyingi zikiwemo kutoka Morocco,” kilisema chanzo.

Hili si jambo jipya kwa Yanga kwani walifanya hivyo kwa Pacome Zouzoua, Kouassi Attohoula Yao na Stephane Aziz KI, ambao mikataba yao ilikuwa ukingoni kumalizika, na wakatumia mbinu hiyo ya kukaa nao mezani kabla ya msimu kumalizika.

Ndani ya misimu miwili akiwa Yanga, Dube amefunga mabao 16 katika Ligi Kuu Bara, huku msimu wa kwanza akimaliza kwa kutia kambani mabao 13. Msimu huu anayo matatu.

Mbali na Dube, Chadrack Boka, Kibwana Shomari na Farid Musa, ni miongoni mwa wachezaji wa Yanga mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu huu.