Ligi Kuu Bara leo zinasakwa pointi tatu za heshima

LIGI Kuu Bara inatarajiwa kuendelea leo Jumanne kwa mechi tatu kupigwa lakini macho ya wengi yataelezwa Uwanja wa KMC jijini Dar es Salaam na mabingwa watetezi, Yanga itashuka dimbani kucheza dhidi ya Dodoma Jiji.

Baada ya kupoteza mechi yake ya kwanza wikiendi iliyopita katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves tangu kukabidhiwa mikoba ya Romain Folz, atakuwa na kibarua kingine cha kurejesha timu hiyo kwenye wimbi la ushindi.

Hii itakuwa mechi ya sita kwa kocha huyo kuiongoza Yanga katika ligi, alianza kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, 4-1 dhidi ya KMC, 2-0 dhidi ya Fountain Gate, 1-0 dhidi ya Coastal Union na 6-0 dhidi ya Mashujaa.

Yanga itaingia katika mechi hiyo ikiwa na mabao 15 kati ya 18 iliyofunga katika ligi chini ya kocha huyo raia wa Ureno, ikiwa na wastani wa kufunga mabao matatu katika kila mechi.

Wakati huo, Dodoma Jiji ambayo imeshinda mechi moja kati ya tano zilizopita, ikiruhusu mabao 10 katika mechi 10 zilizopita, ina wastani wa kuruhusu bao moja kwa mechi huku ikifunga mabao sita tu.

Rekodi inaonyesha katika mechi tano zilizopita ambazo Yanga ilikuwa nyumbani, imeshinda zote huku ikifunga jumla ya mabao 17 na kuruhusu matatu dhidi ya Dodoma Jiji.

Mechi ya mwisho Yanga kuwa nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji ilikuwa Juni 22, 2025 na iliibuka na ushindi wa mabao 5-0 ambayo yalifungwa na Clatous Chama ambaye amerejea zake Simba, Dube Abuya, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Max Nzengeli na moja walijifunga.

Katika mechi hii, Pedro atakuwa akifanya mambo mawili kwa wakati mmoja, kusaka pointi tatu za heshima ambazo zitawafanya kukwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kuishusha JKT Tanzania yenye pointi 21 ikiwa imeshuka dimbani mara 12.

Yanga ipo nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 19, ikishuka dimbani mara saba.

Jambo lingine ni kuhakikisha wachezaji wanakuwa tayari kwa ajili ya kibarua kizito zaidi katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex huko Zanzibar.

Kwa upande wa Dodoma Jiji iliyopo nafasi ya 11, itakuwa ikisaka ushindi wake wa pili mfululizo katika Ligi baada ya kutoka kuichapa Tanzania Prisons bao 1-0.

TRA United iliyovuna pointi tisa katika mechi tano zilizopita, itakuwa na kazi nyingine ngumu ya kufanya dhidi ya Namungo ambayo nayo ipo kwenye kiwango bora kwa sasa kufuatia kushinda mechi tatu mfululizo.

Msimu uliopita, TRA wakati huo ikifahamika kama Tabora United, ilivuna pointi zote sita dhidi ya timu hiyo ya kusini mwa Tanzania, ilianza kwa ushindi wa mabao 2-1 ugenini, pia ikapata matokeo kama hayo nyumbani.

Hivyo hii itakuwa mechi ya kisasi kwa Namungo kufuatia kufanya vibaya msimu uliopita dhidi ya TRA, katika mechi nne ambazo timu hizi zimekutana Namungo imeshinda mara moja tu, ilikuwa Machi 28, 2024 kwa mabao 3-2.

Hii ndio mechi ambayo itafunga pazia kwa leo. Je! kocha Mohamed Bares na vijana wake wa KMC wataiduwaza Coastal Union iliyopo nyumbani kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga au wataendelea kujichimbia shimo mkiani mwa msimamo wa ligi?

KMC inaburuza mkia Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi nne, imeambulia pointi moja tu katika mechi tano zilizopita na ilikuwa Novemba 25, 2025 dhidi ya Mtibwa Sugar.

Kabla ya mechi leo, imekumbana na vipigo viwili mfululizo dhidi ya Pamba Jiji na TRA United vyote kwa mabao 3-0. Licha ya matokeo hayo, KMC imeshinda kufunga hata bao katika mechi nne zilizopita sawa na  dakika 360.

Coastal nao ambao wapo nafasi ya 13 wakiwa na pointi tisa hawapo katika kiwango kizuri, wamechapwa mechi tatu mfululizo dhidi ya Namungo (1-0), Azam (3-0) na Yanga (1-0).