KUMBUKIZI YA KUZALIWA DKT SAMIA: UVCCM KAGERA YAKUPANDA MITI 2,000 SHULE YA WASICHANA OMUMWANI.

Na Diana Byera_Bukoba.

Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kagera wameungana na Rais Samia Suluhu Hassan kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda miti 2,000 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Omumwani, Manispaa ya Bukoba.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM Mkoa wa Kagera, Faris Buruhani, amewaongoza vijana mbalimbali pamoja na wanafunzi na walimu wa shule hiyo katika zoezi la upandaji miti. Shughuli hiyo pia ilihusisha kukata keki na kuimba nyimbo za kumtakia Rais Samia maisha marefu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti Buruhani alisema vijana wa Mkoa wa Kagera wanamuunga mkono Rais Samia na wanampongeza kwa kazi kubwa anayoifanya, ikiwemo kudumisha amani na mshikamano, kuimarisha uongozi bora, pamoja na kusimamia miradi mbalimbali inayogusa jamii kwa ustadi.

Amesema shule ya wasichana Omumwani imechaguliwa kama sehemu ya kuwatia moyo wanafunzi kutimiza ndoto zao katika masomo na kujiandaa kupata nyadhifa mbalimbali za kuwatumikia wananchi siku za usoni, pia aliwaasa wanafunzi kulinda miti iliyopandwa na kuhifadhi mazingira.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Juliana Rukweto, amevutiwa na uongozi wa mwenyekiti pamoja na mshikamano wa vijana, akisema kuwa hafla hiyo imeacha kumbukumbu ya kudumu, aidha, aliahidi kuendelea kuhamasisha wasichana kusoma kwa bidii na kufanikisha ndoto zao.