Miloud Hamdi ajiuzulu Ismaily | Mwanaspoti

Aliyekuwa Kocha wa Yanga msimu uliopita, Miloud Hamdi jana, Jumatatu, Januari 26, 2026 ametangza kujiuzulu kibarua chake katika klabu ya Ismaily ya Misri.

Miloud amechukua uamuzi huo akiwa ameitumikia timu hiyo kwa miezi sita tu tangu alivyojiunga nayo, Julai 3, 2025 akitokea Yanga.

“Nawashukuru kwa nyakati tulizopita pamoja katika vipindi vigumu. Lakini tulifanikiwa kuwa tumeungana pamoja. Tulikuwa familia halisi na wataalam wa tiba na sekretarieti ya klabu ikiongozwa na Ahmed Salah.

“Kufuatia kujiuzulu kwangu klabuni, kipekee nitakumbuka nyakati nzuri pamoja na mashabiki wetu. Nawatakia kila la kheri,” amesema Hamdi.

Japo Hamdi hajaanika sababu za kujiuzulu, mwenendo usioridhisha wa Ismaily chini yake unaweza kuwa chanzo cha Kocha huyo ambaye ni raia wa Algeria na Ufaransa pia kujiweka kando.

Tangu alipoanza kuinoa Julai mwaka jana, Ismaily imepata ushindi katika mechi nne tu kati ya 19 ilizocheza kwenye mashindano tofauti ambapo imetoka sare mbili na kupoteza mechi 13.

Katika mechi hizo 19, timu hiyo imefunga idadi ya mabao 13 huku yenyewe ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 26.

Kocha huyo ambaye amekuwa akipendelea kutumia mfumo wa 4-1-4-1, alijiunga na Ismaily akiwa ametoka kuiongoza Yanga kutwaa mataji mawili makubwa Tanzania ambayo ni Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB.

Hamdi (54) mwenye leseni ya Ukocha ya UEFA Pro, amewahi kuzifundisha pia Singida Black Stars,   Al-Khaldiya, JS Kabylie, CS Constantine, Al Salmiya, Al Ettifaq, RS Berkane na USM Alger.