TRA MOROGORO YAANZA KUTOA MAFUNZO YA IDRAS KWA WALIPA KODI

Farida Mangube, Morogoro

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Morogoro imenza kutoa mafunzo ya matumizi ya Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Kodi za Ndani (IDRAS) kwa wafanyabiashara na walipa kodi 344,712, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuanza kutumika rasmi kwa mfumo huo mpya.

Akizungumza kwenye mafunzo ya IDRIS kwa washauri wa kodi na wahasibu kutoka taasisi mbalimba na Uma na binafsi Meneja wa TRA Mkoa wa Morogoro, Sylver Rutagwelera amewataka kuupokea, kuujifunza na kuuelewa vizuri mfumo wa IDRAS ili kuboresha utoaji wa huduma na kuongeza ufanisi wa makusanyo ya kodi.

Amesema kuwa mfumo huo unatarajiwa kuanza kutumika rasmi Februari 9, 2026 na utasimamia kodi zote za ndani kwa kutumia mfumo mmoja jumuishi unaolenga kurahisisha ulipaji wa kodi na kuongeza mapato ya ndani ya Serikali.

“Tupo katika hatua ya kutoa elimu ya matumizi ya mfumo huu. Tumeanza na watumishi wetu, sasa tupo na wahasibu pamoja na washauri wa kodi kutoka taasisi binafsi na za Serikali. Mafunzo haya yatachukua wiki nzima na baadaye tutahusisha wadau wengine zaidi,” amesema Rutagwelera.

Ameongeza kuwa mafunzo ya awali yaliwahusisha watumishi wote wa TRA wanaohusika na mfumo huo katika mkoa mzima, na sasa elimu hiyo imeanza kutolewa kwa wafanyabiashara katika wilaya zote za Mkoa wa Morogoro.

Rutagwelera amesema baada ya kukamilika kwa mafunzo ya ngazi ya mkoa, timu ya TRA Morogoro itafika katika wilaya zote kutoa elimu hiyo kwa walipa kodi, sambamba na elimu inayotolewa na maofisa wa wilaya, ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anauelewa vizuri mfumo wa IDRAS.

“Tutafanya mafunzo haya hapa ofisini na pia tutawafuata walipa kodi huko walipo hadi pale walipa kodi wote watakapoweza kutumia mfumo huu kikamilifu, kwani tuna walipa kodi 344,712 mkoani Morogoro,” amesema.

Mafunzo hayo yametolewa na Afisa Mwandamizi wa Tehama Ernest Shirima kwa kushirikiana na maafisa wa usimamizi wa kodi John Magembe na Mohamed Mchekaje ambapo wamesema mfumo wa IDRAS utarahisisha zaidi ulipaji wa kodi, kupunguza msongamano wa walipa kodi katika majengo ya TRA na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Mfumo wa IDRAS una moduli 17, ambapo moduli mbili tayari zinafanya kazi tangu mwaka jana, ambazo ni Moduli ya Magari (Motor Vehicle Module) na Moduli ya Leseni za Udereva (Driving Licence Module), Registration, Communication, Return Filing and Assessment, pamoja na Knowledge Management, ambazo zinatarajiwa kutumika hivi karibuni.

Frida Joseph ni moja wa washiriki wa mafunzo hayo mkoani Morogoro, amesema mfumo wa IDRAS utaongeza uwazi na urahisi kwa walipa kodi. “Mfumo huu utapunguza usumbufu wa kufika mara kwa mara ofisi za TRA, na utarahisisha sana kazi yetu ya kuwasaidia walipa kodi kutimiza wajibu wao kwa wakati,” amesema.