CHAMA cha Netiboli Mkoa wa Mbeya (Chanembe) kinatarajia kufanya uchaguzi wa kuwapata viongozi wake watakaokitumikia kwa miaka minne ijayo, huku wadau wa mchezo huo wakiombwa kujitokeza kuchukua fomu.
Uchaguzi huo unatarajia kufanyika leo Jumatano Januari 28, 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, huku nafasi sita zikitangazwa kuwaniwa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama hicho, Veronica Kikalao, amesema uchaguzi huo utakuwa wa huru na haki.
“Nafasi ni sita, ikiwa ni mwenyekiti, makamu, katibu mkuu, katibu msaidizi, mweka hazina na wajumbe sita wa kamati ya utendaji mkoa, hadi sasa taratibu zimekamilika na tunachosubiri ni wagombea kukidhi vigezo,” amesema Veronica.
Aliongeza, sifa za wagombea ni awe anajua kusoma na kuandika, awe na ufahamu wa mchezo wa netiboli, uzoefu wa uongozi, awe na rekodi ya kushiriki shughuli za mchezo huo, hajawahi kuwa kosa la jinai na akili timamu.
Amesema fomu zilianza kutolewa tangu Januari 24, 2026 kwa Sh20,000 na Sh10,000 kwa nafasi za wajumbe na mwisho wa kurejesha ilikuwa jana Januari 27, 2026.
Kwa upande wake, Afisa Michezo Mkoa wa Mbeya, Robert Mfugale amesema uchaguzi huo ni muhimu ili kupata uongozi mpya baada ya uliokuwapo kuisha muda wao tangu Oktoba 2025.
“Ni uchaguzi wenye baraka kwakuwa unaandaliwa na kusimamiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, lengo si kuwahi uchaguzi wa mchezo huo Taifa bali kupata viongozi watakaosimamia mchezo huo maeneo yote ya Mkoa.
“Kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya Wilaya kutokuwa na hamasa ya kucheza Netiboli, hivyo kupatikana kwa viongozi itasaidia kusimamia uhai wa Netiboli kwa maeneo yote,” amesema Mfugale.