UNAWEZA kujaribu kuukimbia ukweli lakini wengine wakausema kama ambavyo kocha mmoja wa zamani wa Simba amekubali yaishe akiweka hadharani kwamba watani wao Yanga wamerudi kwenye ubora wao kwa kuwa na timu nzuri.
Aliyeyasema hayo ni kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ambaye ametulia na kuziona timu zote mbili kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika akisema Yanga imerudisha ubora wa timu yao ya misimu miwili iliyopita.
Robertinho amesema Yanga ilikuwa kama inapepesuka lakini kwa usajili walioufanya hivi karibuni wamekwenda kukiimarisha kikosi chao na kurudi kwenye ubora mkubwa.
Kocha huyo raia wa Brazil, amesema kama Yanga itaendelea kuwa pamoja kwa miezi sita ijayo itakuwa na timu ngumu zaidi kufungika kwani maboresho ya kikosi chao yanafanyika kwa hesabu sahihi.
“Kuna wakati nilikuwa naona kama wanaanza kupotea, nilipata wasiwasi lakini kuna wachezaji wamewaongeza hivi karibuni naona kabisa wamerudi kwenye ubora wao halisi,” amesema Robertinho.
“Timu yao imekamilika, imewekwa kwenye mzani sawa, wachezaji waliowaongeza wana nguvu kubwa ukiwaunganisha na wale waliokuwepo kama watakaa vizuri watakuwa bora zaidi, kitu ambacho nakiona wanakuwa na hesabu nzuri kwenye kujenga timu yao.
“Kama wataendelea kucheza hivi wanaweza kufanya vizuri zaidi, sitashangaa kuona wanakwenda robo fainali ya ligi ya mabingwa, wanacheza kama timu moja na kocha wao mzuri.”
Aidha akiizungumzia Simba, Robertinho amesema bado mashabiki wa timu hiyo wanatakiwa kusubiri kuona uhalisia wa mabadiliko ya kikosi chao ambacho ni kama kipya kikiwa na kocha mpya na wachezaji.
Hadi sasa Simba imesajili wachezaji wapya sita wakiwemo kipa Djibrilla Kasali, mabeki Nickson Kibabage, Ismael Toure na viungo Libasse Gueye, Clatous Chama na Anicet Oura.
“Ni vigumu kutoa tathimini kwa Simba, bahati mbaya sana bado kuna mambo ya kusajili kikosi yanaendelea, mpaka sasa nimeona wameongeza wachezaji watano (kabla ya kusajiliwa kwa Oura) hiyo ni kama nusu ya timu.
“Bado tena unaona kuna makocha wapya, haya yote naona yanahitaji mashabiki kusubiri kwanza kuona kocha atawaunganisha vipi na kuleta matokeo ya timu kucheza kwa ushindi,” amesema kocha huyo.
Wakati Simba ikitambulisha wachezaji wapya sita, Yanga kupitia dirisha dogo imeingiza wachezaji wapya watano ambao ni kipa Hussein Masalanga, kiungo mkabaji Mohamed Damaro, winga Allan Okello na washambuliaji Emmanuel Mwanengo na Laurindo Dilson Maria Aurelio maarufu Depu.
Robertinho aliinoa Simba kuanzia Januari 3, 2023 hadi Novemba 9, 2023 ambapo anakumbukwa kuwa ndiye kocha wa mwisho kuifunga Yanga, akifanya hivyo mara mbili kati ya tatu.
Alianza na ushindi wa 2-0 katika Ligi Kuu Bara mechi ikichezwa Aprili 16, 2023, kisha penalti 3-1 katika fainali ya Ngao ya Jamii (Agosti 13, 2023). Kipigo alichopokea Novemba 5, 2023 kutoka kwa Yanga cha mabao 5-1, ndicho kilihitimisha safari yake Msimbazi.
Baada ya hapo, akatimkia Rayon Sports, kisha Jeddah SC ya Saudi Arabia alipo sasa.