Miaka 33 ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imekuwa na chungu tamu kadhaa ambazo wenyewe wanasema zimekijenga na kukiimarisha chama hicho kwa viwango vya juu hadi kuaminiwa na Watanzania.
Kikiwa ni moja ya vyama 19 vyenye usajili wa kudumu nchini, Chadema ndiyo chama chenye mvuto wa kisiasa kwa sasa, kikiwa na sera na mikakati inayoungwa mkono na wananchi wengi hasa kwenye miji mikubwa.
Hata hivyo, chama hicho kimekuwa kikipitia dhoruba miaka ya hivi karibuni ikiwamo zuio la kuendesha shughuli zake za kisiasa na kuziliwa kwa ruzuku ambayo kimekuwa kikiipata kwa mujibu wa sheria.
Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Chadema, Gervas Lyenda ambaye amezungumzia masuala mbalimbali ikiwamo kampeni ya ‘No reforms, No election’ iliyokuwa ikiendeshwa na chama hicho.
Kampeni ya ‘No reforms’
Chadema kilianzisha kampeni ya No reforms, No elections (bila mabadiliko hakuna uchaguzi) kwa lengo la kushinikiza mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi ikiwamo kwenye Tume ya Uchaguzi.
Chama hicho kupitia kwa mwenyekiti wake, Lissu, kilianza ziara kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, hata hivyo Lissu alikamatwa na kampeni hiyo ikasimama hasa kufuatia kesi ya mgawanyo wa mali iliyofunguliwa mahakamani na kusababisha zuio la kutumia mali za chama.
Kuhusu mustakabali wa kampeni hiyo, Lyenda anasema Kamati Kuu ya chama hicho bado haijakaa kujadili jambo hilo kwani ndiyo yenye uamuzi wa mwisho kwenye jambo lolote ikiwemo kampeni ya “No reforms, no election”.
Anaeleza kwamba ajenda hiyo bado ipo hai, ingawa mwelekeo wa utekelezaji wake utajulikana baada ya vikao rasmi kukaa na kuja na msimamo wa pamoja.
Lyenda anasema mabadiliko wanayoyataka bado hayajatekelezwa, hivyo wanaamini uchaguzi hauwezi kufanyika kwa haki bila marekebisho hayo. Hatua zitakazofuata zitasubiri uamuzi wa vikao vya chama.
Pamoja na kuendesha operesheni mbalimbali ikiwemo ya ‘No reforms, No election’, anasema lengo kuu la chama ni kushika dola, wakiamini kuwa kwa sasa wako imara zaidi na wanaungwa mkono na wananchi kuliko hapo awali.
“Ndiyo maana tunasema Chadema ni chama kikuu cha upinzani Tanzania. Licha ya misukosuko mikubwa, tumeendelea kusimama imara hatujatoka katika dhamira yetu,” anasema.
Anahoji iwapo chama tawala kinaungwa mkono, kwa nini kinachagua waamuzi wa mchakato wa uchaguzi badala ya kushindana kwenye uwanja wenye usawa.
“Kwanini tusicheze kwenye uwanja tambarare? Kama wanataka haki, basi kuwe na uwazi katika chaguzi,” anasema.
Anaongeza kuwa Chadema tayari kimeonyesha mfano kupitia uchaguzi wake wa ndani wa Januari 21, 2025 ambapo mchakato mzima ulirushwa mubashara kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
“Uwazi unaleta haki. Hata anayeshindwa anaridhika kwa kuwa anaona mchakato mzima,” anasema.
Kwa mujibu wake, chama kiko katika mwelekeo wa kushika dola na hakitishwi na changamoto, kwani wanaamini nyakati ngumu hazidumu.
Anasema kampeni ya No refors, no Election imekuwa na mafanikio makubwa kuliko walivyokuwa wanafikiria awali, kwani imekuwa kubwa kuliko zote zilizowahi kufanyika ndani ya chama hicho tangu kuanzishwa kwake.
“Tuliwahi kuwa na opresheni Sangara, tukaja kuwa na Movement For Change (M4C) na ikaja ya No reforms, No election, operesheni ambazo zinaanzishwa kwa lengo la kujenga chama,”anasema,
Anasema kupitia operesheni hizo huwa wanawatembelea wananchi kuwashawishi kukiunga mkono chama hicho lakini No reforms no election imekuwa na mafanikio makubwa ingawa ilileta mgawanyiko ndani ya chama.
“Ilianza rasmi Machi 23, kwa Mwenyekiti Lissu kuongea na waliokuwa wanataka kuwania Ubunge, Udiwani na Urais, na alisimamia kama hakuna mabadiliko hatutaenda kushiriki uchaguzi,”anasema
Anasema baada ya kikao hicho walienda kuanza mikutano Kanda ya Nyasa yenye mikoa mitano ikiwemo Mbeya, Njombe, Songwe, Rukwa, Katavi baada ya kumaliza walihamia Kanda ya Kusini.
“Tulipoingia Kanda ya kusini tulifanya mikutano lakini baadaye Mwenyekiti wetu alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uhaini, lengo ilikuwa kutuziba mdogo kwakuwa tulikuwa tunatoa elimu ya kuwafungua akili wananchi,”anasema.
Anasema pamoja na kukamatwa Lissu, viongozi wengine waliendelea na mikutano hiyo kabla ya kufunguliwa kwa kesi nyingine, chama kikazuiwa kufanya siasa na ukawa mwisho wa kampeni hiyo.
“Ndani ya muda wa miezi miwili iliyofanyika ujumbe ulikuwa umefika kwa Watanzania, na kile ambacho walikitarajia walifanikiwa baada ya Chadema kutoa elimu na watu walielewa haki yao,” anasema.
Licha ya misukosuko ya nje, ndani ya chama kulikuwa na mgawanyiko mkubwa kuhusu kampeni hiyo huku akitumia msemo kuwa kwenye msafara wa mamba na kenge nao hawawezi kukosekana.
“Baada ya mwenyekiti kutoa msimamo kuhusu Operesheni anamaanisha wale wanasiasa uchwara na wapiga dili waliondoka Chadema kwa sababu walikuwa wanaona wahawezi kupata wanachotaka,” anafafanua.
Kada huyo wa Chadema anasema waligawanyika kiasi cha kuhamia vyama vingine ikiwemo vya upinzani, hawakuwa na dhamira ya kupigania malengo ya chama bali walikuwa wanajiangali wao.
“Walikuwa hawataki demokrasia itamalaki kwenye nchi yetu, wanafikiria wao kushika vyeo ndiyo maana watu hao waliondoka,” anasema Lyenda.
Katika miaka 33 tangu kuanzishwa kwa Chadema, Lyenda anasema chama hicho kimefanikiwa kuleta mageuzi ya kisiasa na kuwa chama madhubuti kinachokipa changamoto chama tawala cha CCM.
Lyenda anasema Chadema kimekuwa kikitengeneza sera mbadala zinazokubalika kwa wananchi. Anasema uimara wake unakilazimisha chama tawala kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yake, kwa kutambua kuwa upinzani upo tayari kuhoji na kutoa ushindani kwenye chaguzi.
“Uwepo wetu kama chama imara unakifanya chama tawala kuwa makini wakati wote, kwa kuwa wanajua wakikosea, chama cha upinzani kitasimama na kuzungumza pamoja na kutoa ushindani mkubwa wakati wa uchaguzi,” anasema.
Anasema Chadema kimechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi kupitia sera mbadala ambazo baadaye zimekuwa zikichukuliwa na chama tawala, ingawa utekelezaji wake haujafanyika kwa ufanisi kama wao walivyokusudia.
“Mathalani, suala la elimu bure lilikuwa ni wazo la Chadema lililowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010, wakati mgombea wetu wa urais alikuwa Dk Wilbrod Slaa. Tulipanga tukishika dola, elimu iwe bure,” anasema.
Kwa mujibu wa Lyenda, mwaka 2020 chama tawala kilikuja na wazo hilo hilo la elimu bure, hata hivyo anasema halijatekelezwa kwa mifumo waliyoikusudia awali, kwa kuwa hawakuwa waanzilishi wa mpango huo.
Anaeleza Chadema kiliwahi kuzungumzia suala la bima ya afya kwa wote, na kwa sasa Serikali inaendelea kutafakari uwezekano wa kuanzisha mpango huo.
“Chadema kimefanya mambo mengi katika kulijenga Taifa. Tunakuja na mawazo, tunayapambania katika ilani za uchaguzi, na mara nyingi Serikali huyachukua na kuyafanyia kazi,” anasema.
Lyenda anasema katika kipindi cha miaka 33, chama hicho kimepitia changamoto nyingi zikiwemo machungu ya kupoteza baadhi ya makada wake waliokuwa mstari wa mbele katika harakati za kisiasa, baadhi wakitekwa, kupotezwa na wengine kuuawa.
“Wapo walionusurika katika majaribio ya kuuawa, akiwemo mwenyekiti wetu wa sasa, Tundu Lissu ambaye alipigwa risasi nyingi. Mwili wake umeathirika na hadi sasa hawezi kutembea vizuri,” anasema Lyenda.
Anasema chama hicho kilifungiwa kufanya shughuli za kisiasa, akaunti zake kufungwa na kuzuiwa kutumia mali zake, hali aliyosema imekuwa ngumu kwa uendeshaji wa chama.
“Imetuathiri na kuna wafanyakazi walikuwa wanafanya shughuli zao makao makuu, walikuwa wanapata posho lakini kwa sasa tunashindwa kuwalipa kwa sababu akaunti zimefungiwa,” anasema ofisa huyo wa Chadema.
Anaongeza kuwa pamoja na ugumu huo, chama hicho kimekuwa kikiendeshwa kwa michango ya watu, na kukiwa na jambo wanalipeleka kwa wananchi kuwaeleza kwamba wana changamoto ya kifedha.
“Pamoja na kutuchangia fedha hizo, tunashindwa kuzipokea kupitia akaunti za chama wala namba za simu za chama, ndiyo maana wamekuwa wakiomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa chama kupitia namba ya kiongozi mmoja wapo,” anasema.
Kwa mujibu wake, pamoja na jitihada hizo mbaya zaidi kupitia mifumo ya mitandao ya simu imekuwa ikiwahujumu kwani hata namba wanazoweka, mitandao hiyo imekuwa ikizifungia wanajaribu kulalamika na hawapewi majibu.
“Tunashughulikiwa kwa kila namna, hata namba binafsi tunazoweka nazo pia zinafungiwa, inakuwaje tunafungiwa, hawaelezi sababu ni nini,” anasema.
Lyenda anasema Chadema kimekuwa ni chuo la viongozi wengi mahiri nchini, akieleza kuwa hata waliokihama chama hicho wameendelea kung’ara katika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini na katika vyama vingine vya siasa.
Anatolea mfano wa Kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, aliyewahi kuwa mwanachama wa Chadema kabla ya kuanzisha chama hicho na kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa kitaifa.
“Wengine ni Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, pamoja na Patrobas Katambi, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye awali alikuwa Mwenyekiti wa Bavicha. Hawa ni zao la Chadema,” anasema.
Anasema wanasiasa wengine waliotokana na Chadema ni pamoja na David Silinde, Naibu Waziri wa Kilimo, Halima Mdee, Peter Msigwa, Juliana Shonza na Mwita Waitara, akisema wote wamekuwa na mchango mkubwa ndani na nje ya Bunge.
“Ndani ya miaka 33, Chadema kinajivunia kuzalisha viongozi mahiri, jasiri na wachapakazi kwa ajili ya Taifa letu,” anasema.