NIKWAMBIE MAMA: Kodi ni maji kwenye tenga?

Mwili wa kiumbe hai ni kitu cha ajabu sana. Kama vuimbe hai tusingelikuwa na ngozi, au tungekuwa na mwili wa kioo inayoonesha yanayoendelea huku ndani, nadhani hata wenyewe tungeogopana. Macho yangeona tonge la ugali linavyomezwa kooni, linavyoshuka kusagwa tumboni na kadhalika. Mtu angeshindwa kuongopa kuwa amekula kuku wakati kisamvu na maharagwe vinaonekana tumboni.

Pamoja na kuwa viungo vya mwili ni vingi na visivyo na idadi, mwili una mawasiliano na kila kila kiungo chake hata kiwe kidogo kwa kiasi gani. Mamilioni ya taarifa yanatolewa, kupokelewa na kufanyiwa kazi katika muda mfupi sana. taarifa zinafanyiwa upembuzi na kutolewa maamuzi ndani ya muda huo huo. Iwapo kiungo kimoja kitazembea japo kwa nukta moja tu, kiumbe atapoteza maisha katika nukta hiyo hiyo.

Chukua mfano wa mtu anayesinzia akiota moto. Katika usingizi wake anahisi kuna jambo haliko sawa mwilini. Ngozi inatuma mishipa ya fahamu kuulizia kwenye ubongo. Ubongo unauchakata mwili na kupata jibu kuwa ni kipande cha moto kutoka kwenye kuni kimerukia mguuni. Kufumba na kufumbua, ubongo unaiamuru misuli ya mkono kukiwahi kipande cha moto kabla hakijaleta madhara zaidi. Mambo haya huacha kufanyika pale tu mtu anapokuwa amekumbwa na umauti.

Vinginevyo hata angelala fofofo, viungo vya mwili vinavyolala huwa vichache ukilinganisha na vile vinavyokesha.

Huku mtaani kuna watu hawawezi kuamka mpaka wapate pegi ya kinywaji kikali. Wenyewe wanasema “kutoa loki”. Hawa huwa mashahidi wa uadilifu wa viungo vya mwili, kwani anapomeza funda la kikali tu na haja ndogo inamshika palepale. Haya ni matokeo ya figo kugundua kuwa imeingiliwa na sumu.

Haraka figo inatoa taarifa kwa ubongo, nao unaamuru yatafutwe maji popote mwilini kwenda kuitoa sumu hiyo kabla haijaleta madhara makubwa.

Hivi ndivyo Serikali yoyote inavyotakiwa kufanya kazi. Moja ya shughuli muhimu za Serikali ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Nchi haiwezi kuwa nchi bila huduma bora za kijamii. Hivyo Serikali yoyote iliyopo madarakani hutumia kila raslimali iliyopo kuendeleza nchi, ilimradi wananchi wapate hali bora za kimaisha. Ujenzi wa shule, hospitali na miundombinu huwa ni sehemu ya vipaumbele vikubwa vya Serikali.

Serikali haina budi kutafuta vyanzo vya fedha kufanya maendeleo ya watu wake. Vyanzo vikuu kwa nchi inayojitegemea ni vile vya ndani vikiwemo makusanyo ya kodi. Lakini pia hutegemea mauzo ya ndani na nje ya bidhaa zake, raslimali za Taifa kama utalii na kadhalika. Inapotokea vyanzo hivyo kutofikia kiwango cha kutosha, mikopo na misaada huingia kuziba pengo.

Kwa sasa hakuna asiyejua kuwa tunapita kwenye wakati mgumu sana, hasa wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025. Baadhi ya wahisani wetu hawajakubaliana nasi kiasi cha kupunguza au kusimamisha misaada na mikopo yao. Tegemeo kubwa tulilonalo hivi sasa ni fedha za ndani, ambazo kwa ukweli hazitoshelezi kuanzisha, kuendeleza au kumalizia miradi mikubwa ya maendeleo.

Katika hotuba yako ya kwanza mara baada ya uchaguzi, ulilisema jambo hili japo halikueleweka vizuri. Lakini majukumu uliyowapa Mawaziri baada ya kuwateua yalilenga zaidi kutafuta fedha za ndani kokote zilipo ili mambo yaende. Hapa sasa ndipo mifumo ya Serikali inapolazimika kufuata muundo wa mfumo wa mwili wa kiumbe hai. Kimoja kikizembea, kiumbe kizima kinashindwa kutoboa.

Nilimsikiliza Waziri Mkuu katika hotuba yake ya uzinduzi wa meli ya MV Mwanza. Moja kero alizozipokea na kuziongelea ni kusimama kwa miradi ya maendeleo. Hili limetajwa kwa kiasi kikubwa kusababishwa na kukosekana kwa fedha za awali zakuwalipa wakandarasi. Waziri alisema hatuna budi kugharamia kimkakati miradi ya maendeleo ya kimkakati. Kugharamia kunamaanisha kutekeleza miradi kwa fedha zetu wenyewe. Kwa macho ya nyama, fedha hizi haziwezi kuonekana. Zitatoka wapi kwenye nchi masikini kama hii? Tangu lini watu wanaoshindwa kuwawekea watoto wao madaftari shuleni, wakaweza kutekeleza miradi mikubwa ya maji na ujenzi wa viwanja vya ndege? Kwa upande huu, hizi sawa na ndoto za Alinacha. Huyu bingwa alitegemea kuwa bilionea na mkwe wa Sultani kwa mtaji wa kuchuuza vikombe barabarani.

Lakini kwa fikra halisi, hili ni jambo linalowezekana pasi na shaka yoyote. Iwapo kila mmoja atasimama vema kwenye nafasi yake, hakuna jambo litakaloshindikana. Huu ndio wakati wa kila mtu kujiuliza mwenyewe kwa nini alichagua nafasi aliyopo. Kama alisimama jimboni kuomba ridhaa ya wananchi, ndio wakati wa kuthibitisha kuwa alikijua kile alichoomba. Hili linamhusu yeye kama yeye.

Waziri Mkuu aliagiza kuachana na maisha ya mazoea. Kuna maisha ya Taasisi za Serikali kutumiana kalenda, shajara na hata vifurushi vya zawadi kila msimu. Alitoa mfano wa mtu anayewasha kiswaswadu na kujua tarehe ya siku husika, je mtu huyo analazimika kuchapishiwa kalenda ya gharama? Ataitazama saa ngapi wakati muda wote yupo kwenye simu? Au kama anahitaji mapambo si akayanunue mwenyewe?

Kile alichokiona Waziri Mkuu ndiyo matundu makubwa ya kodi za wananchi. Angeangalia mbele zaidi angeyaona mafriza ya wakuu yanayojazwa kwa kodi hizihizi za mamantilie!