Kwa muda mrefu, dunia imekuwa ikiyumba kati ya nguvu za watawala binafsi wenye nguvu za kijeshi, kiuchumi na kisiasa, na juhudi za kujenga mifumo ya sheria za kimataifa inayolenga kutoa mwelekeo wa pamoja wa dunia.
Kabla ya karne ya 20, nguvu za kijeshi, kiuchumi au ushawishi wa kisiasa ziliwezesha mataifa au watu wachache wenye nguvu kuamua mwelekeo na hatma ya dunia bila kuwepo mfumo wa juu wa kimataifa wa kuwadhibiti. Kipindi hicho hakikuwa na taasisi za pamoja kama zilizopo leo.
Maafa ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia yalibadilisha fikra hizo. Dunia ilitambua kuwa kumuacha mtu mmoja au taifa moja kuendesha mambo ya kimataifa bila vizuizi ni hatari kwa amani na utulivu wa dunia.
Hapo ndipo Jumuiya ya Mataifa (League of Nations) ilipoanzishwa na baada ya kushindwa kwake, Umoja wa Mataifa (UN) ukaasisiwa mwaka 1945 kama nguzo ya mfumo wa sheria za kimataifa.
Lengo lilikuwa kuondoa uwezekano wa mtu au taifa moja kuamua mustakabali wa mataifa au watu wengine.
Leo karibu miaka 80 tangu kuundwa kwa UN, dalili zinaonyesha mpasuko mkubwa duniani. Migogoro ya kijeshi, vita vya kiuchumi, kudharauliwa kwa maamuzi ya kimataifa na kuimarika kwa viongozi wenye mamlaka binafsi vinaibua hofu ya dunia kurejea kwenye zama za uamuzi wa mtu mmoja kwa sura mpya.
Donald Trump, Rais wa Marekani aliyeingia Ikulu ya White House kwa mara ya pili mwaka 2025, alikuta nchi yake ikiwa mhimili mkuu wa mfumo wa UN na taasisi za kimataifa.
Rais wa Marekani, Donald Trump
Trump ameitangaza hadharani UN kuwa haifanyi kazi, akapunguza ufadhili kwa taasisi zake na kuiondoa Marekani kwenye mikataba muhimu ya kimataifa ikiwemo, Unesco na WHO, akipinga falsafa ya dunia inayoongozwa na sheria za pamoja, akitumia ushuru na vikwazo kama silaha za kisiasa bila ushauri wa kina na washirika wake wa kimataifa.
Hatua zake za kuchukua uamuzi wenye athari za kimataifa bila kujali misingi ya sheria za kimataifa ikiwemo kuivamia Venezuela na kumkamata kiongozi wakemkuu,mkakati wake kuivamia Greenl;and na Canada zinadhihirisha mfano hatari kwamba taifa lenye nguvu linaweza kuendesha dunia bila kuwajibika kwa mfumo wa pamoja.
Vladimir Putin, Rais wa Urusi, anawakilisha upande mwingine wa mtazamo huo. Ameendelea kupuuza maazimio ya jumuiya za kimataifa katika uvamizi wa Ukraine, akidai ni hatua ya kulinda usalama wa taifa lake.
Rais wa Russia, Vladimir Putin
Tangu aingie madarakani mwishoni mwa miaka ya 1990, Putin ameijenga Urusi kama dola isiyojifunga na sheria za baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Uvamizi wa Georgia, Crimea na baadaye Ukraine umevunja kanuni za uhuru wa mataifa na mipaka ya kimataifa.
Xi Jinping wa China anaendesha mkondo unaofanana lakini kwa athari za muda mrefu zaidi. Ndani ya China, amevunja mifumo ya uongozi wa pamoja na kujikusanyia mamlaka makubwa ya mtu mmoja.
Kimataifa, China imepinga uamuzi wa mahakama za kimataifa kuhusu Bahari ya China Kusini, huku ikijenga mfumo mbadala wa ushawishi kupitia mikopo, biashara na miundombinu, hali inayopunguza uzito wa UN kwa mataifa mengi.
Rais wa China, Xi Jinping
Kwa pamoja, Trump, Putin na Xi wanaonesha mwelekeo hatari wa kudhoofisha taasisi za kimataifa na kurejesha maamuzi makubwa ya dunia mikononi mwa watu binafsi au mataifa machache yenye nguvu.
Historia inaonesha katika karne ya 20, watawala wenye nguvu waliweza kuipa dunia mwelekeo waliotaka bila kuzuiwa na sheria za kimataifa.
Otto von Bismarck, Kansela wa kwanza wa Ujerumani iliyoungana (1871–1890), alitumia nguvu za kijeshi na diplomasia kuibadilisha Ulaya. Mkutano wa Berlin wa 1884–1885 uliogawa Afrika bila Waafrika kushirikishwa uliathiri mamilioni ya watu kwa vizazi.
Adolf Hitler alivunja mfumo dhaifu wa Jumuiya ya Mataifa, akavunja mikataba ya kimataifa na kuisukuma dunia kwenye Vita Kuu ya Pili iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 60.
Joseph Stalin wa Umoja wa Kisovieti alitawala hadi 1953, akitumia nguvu za kijeshi na kiitikadi kudhibiti Ulaya Mashariki bila chombo cha kimataifa chenye uwezo wa kumzuia, akiweka msingi wa Vita Baridi na hofu ya nyuklia iliyodumu hadi leo.
Wakati dunia ikielekea kutawaliwa na mataifa yenye nguvu na kusitisha ufadhili kwa taasisi za kimataifa, wachambuzi wasiasa na uchumi wanaitazama Afrika kama mwathirika asiye na uwezo wa kujinasua na madhara ya mivutano hiyo inayoyumbisha mwelekeo wa dunia wakisema kukosekana kwa umoja na vyomboi vyenye nguvu barani Afrika kwenye kusimamia mambo yake kunaliweka bara hilo kwenye hatari zaidi.
“Afrika inao umoja wa afrika (AU), lakini haina umoja, kila nchi imebaki kulinda uhuru wake zaidi bila kuwa na umoja wa bara zima katika kutetea maslahi ya pamoja.
Afrika haijawa na jumuiya imara za kusimamia na kutatua mambo yake bila kutegemea nje,” amesema, Profesa Issaq Shivji, Mhadhiri mwandamiziwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Kwa wachumi, nao wanatahadharisha kuwa uchumi wa dunia unaweza kuyumba kutokana na mivutano hii wakitoa wito kwa mataifa yasiyo na uchumi imara yakiwemo ya Afrika kuwekeza katika diplomasia ya maarifa na wataalamu ili kuepuka kuingia kwenye utegemezi wa misaada inayoweza kugeuka kitanzi kwa mamlaka na uhuru baadaye.
Ibara ya 5 ya Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Atlantiki ya Kaskazini (NATO) ndiyo msingi mkuu wa dhana ya ulinzi wa pamoja inayoliunganisha kundi hilo la kijeshi.
Ibara hiyo inaeleza wazi kuwa shambulio la kijeshi dhidi ya nchi moja mwanachama wa NATO litachukuliwa kama shambulio dhidi ya wanachama wote.
Na ikumbukwe, Ibara ya 5 ilianzishwa rasmi mwaka 1949 chini ya Mkataba wa Washington, ulioasisi NATO baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, katika mazingira ya wasiwasi wa kiusalama barani Ulaya na kwingineko.
Kihistoria, ibara hiyo imetumika rasmi mara moja tu, kufuatia mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, 2001 dhidi ya Marekani, ambapo NATO ilitangaza kuwa mashambulizi hayo yalihesabika kama shambulio dhidi ya wanachama wote wa muungano huo.
Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN Charter) unaweka msingi wa kisheria unaoongoza uhusiano kati ya mataifa huru duniani, kwa lengo la kulinda amani na usalama wa kimataifa. Kiini cha misingi hiyo kinajidhihirisha katika Ibara ya 2(4), inayolenga kuzuia matumizi ya nguvu, vita na uvamizi kati ya nchi wanachama.
Licha ya uwazi wake wa kisheria, utekelezaji wa Ibara ya 2(4) umeendelea kukumbwa na changamoto kubwa katika siasa za kimataifa. Ukiukwaji wake hujitokeza pia kwenye uvamizi wa kijeshi wa moja kwa moja. Nchi inapovuka mipaka ya taifa jingine na kuingiza majeshi yake bila idhini ya UN, kitendo hicho hutafsiriwa kama ukiukwaji wa wazi wa Ibara ya 2(4).