Hivi ndivyo unavyoweza kununua mke, mume sokoni China

Inaweza kuwashtua wengi, lakini nchini China yapo masoko ya ndoa halisi ambako wazazi na wakati mwingine watu binafsi hukusanyika kutafuta waume au wake kwa watoto wao.

Katika miji mikubwa kama Shanghai, Beijing na Guangzhou, masoko hayo hufanyika kwenye bustani za umma, hususan mwishoni mwa wiki.

Wasichana wakisoma matangazo ya uchumba yaliyobandikwa kwenye kamba katika soko maarufu la wachumba lililopo katika Jiji la Shanghai, China. Soko hilo lilianza mwaka 2004 katika eneo lililokuwa uwanja wa zamani wa mbio za farasi. Picha na Mtandao



Kwenye bustani hizo, huonekana mistari ya mabango yaliyoandikwa kwa mkono au miamvuli iliyofunguliwa, kila mmoja ukiwa na taarifa za muhusika ikijumlisha umri, urefu, kiwango cha elimu, kazi, mshahara, mji wa asili, pamoja na iwapo anamiliki nyumba au gari. Pia kunakuwa na picha, ukiangalia sifa hizo zinafanana na wasifu wa ajira   kuliko wasifu wa kutafuta mchumba.

Kwa mujibu wa Jarida la Diplomat kinachovutia zaidi ni kwamba, mara nyingi watu wanaotangazwa hawapo eneo hilo. Badala yake, wazazi huja kwa niaba ya watoto wao watu wazima, wakitumaini kuwasaidia kupata wenza wanaofaa.

Wageni wanaotembelea soko la kununua wachumba katika eneo la People’s Square, Shanghai, China wakitazama matangazo ya kutafuta wachumba yaliyobandikwa sokoni hapo. Picha na Mtandao



Katika jamii ambako ndoa bado inaonekana kuwa hatua muhimu ya maisha, na presha ya kifamilia inaweza kuwa kubwa, masoko haya huonekana kama njia ya vitendo, si jambo la ajabu.

Masoko ya ndoa yameibuka kutokana na hali za maisha ya kisasa: saa ndefu za kazi, gharama kubwa za makazi, na programu za kutafuta wachumba mtandaoni ambazo mara nyingi hazileti mahusiano ya kudumu.

Kwa kizazi cha wazee, njia hii ya kukutana ana kwa ana na inayotegemea takwimu huonekana kuwa ya kuaminika zaidi kuliko kutumia simu au mitandao ya kijamii.

Mwanaume aliyefahamika kwa jina la Tsai akibadilishana namba za simu na Hu ili kuwaunganisha watoto wao kwa lengo la uchumba. Picha na Mtandao



Ingawa vijana wengi wa China wanaahirisha ndoa au kuamua kutooa kabisa, masoko haya bado yanaendelea kuwepo, yakichanganya mila za jadi na mbinu za kisasa za ulinganishaji wa wachumba.

Baadhi ya wanandoa wameripotiwa kukutana na kufunga ndoa kupitia masoko haya, huku kwa wengine yakibaki kuwa ishara ya mvutano kati ya uhuru wa mtu binafsi na matarajio ya kitamaduni.