Dodoma. Mbunge wa Kinondoni (CCM), Tarimba Abbas amesema Serikali haioni haja ya kuweka sharti la kisheria la watoto wakubwa kuwatunza wazazi wao wasiojiweza.
Hii ni mara ya pili hoja hiyo kuibuka bungeni , kwani katika Bunge la 12, hoja kama hiyo iliibuliwa na aliyekuwa Mbunge wa Kahama Mjini (CCM), Jumanne Kishimba ambaye alitaka itungwe sheria kwa ajili ya kuwabana watoto wawatunze wazazi wao.
Kishimba wakati wote alikuwa akilalamika kuwa, Serikali haiwapi faraja wazazi kwani inachukua watoto wakiwa wadogo na kuwaanzisha shule, lakini inawarudisha majumbani wakiwa na vyeti huku hawajui kuchunga wala kulima na kuwafanya wawe mzigo.
“Si hayo tu mheshimiwa Spika, hawa watoto hawawatunzi wazazi wao badala yake wanataka kuhudumiwa na wakati mwingine utakuta wazazi wameshachoka hawawezi, lakini walivyotafuta vinaliwa na watoto ambao mwisho wanakimbilia mijini, naomba iletwe sheria hapa tupitishe amri ya wazazi kutunzwa na watoto wao,” aliwahi kupendekeza Kishimba na kuibua shangwe kwa wabungeni.
Leo Jumatano Januari 28,2025 akizungumza bungeni, Tarimba amesema katika mataifa mengine kuna sheria za lazima kwa watoto kuwalea wazazi wao lakini Tanzania ina sheria ya lazima kwa wazazi kuwalea watoto, hivyo akaomba ipelekwe haraka bungeni sheria hiyo ili iwalazimishe watoto kuwatunza wazazi wao. Huku akipendekeza pia Serikali ikajifunze hilo kwenye mataifa yanayotumia sheria hiyo namna inavyofanya kazi.
Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto, Maryprisca Mahundi amesema Serikali inatambua umuhimu wa familia na jamii kuchukua jukumu la kulea wazee.
Mahundi amesema huo ndio msingi wa mila na desturi za Watanzania na jukumu hili ni msingi unaojengwa katika hatua za awali katika malezi na makuzi ya watoto.
“Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha huduma na matunzo kwa wazee, Serikali imefanya mapitio na kutunga Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003, Toleo la Mwaka 2024. Sera hiyo inatoa wajibu kwa familia na jamii kusimamia matunzo ya wazazi,” amesema Mahundi.
Amesema sera hiyo imeweka msisitizo wa kuimarisha mfumo wa kisheria utakaolinda na kuendeleza wazee ambao utawezesha uwajibikaji wa jamii na watoto kuwatunza wazee wao.
Amefafanua kwa sasa Serikali ipo kwenye hatua ya kuwashirikisha wadau ili kutoa maoni juu ya umuhimu na masuala muhimu ya kuzingatiwa katika sheria hiyo.
“Napenda kutoa wito kwa wazazi kuwekeza kwenye malezi ya watoto na siyo matunzo peke yake kwani inaendeleza ukaribu na muunganiko imara kati ya wazazi na watoto. Mzazi anapobeba jukumu la malezi na matunzo ya watoto wake kikamilifu hujenga msingi imara kwa mtoto kumuhudumia anapozeeka,” amesema.
Kuhusu Tanzania kwenda kujifunza katika mataifa ambayo yanatumia sheria ya lazima kwa watoto kuwatunza wazazi wao, amesema Serikali itajifunza huko na itakuja na mapendekezo kama itaona kuna ulazima.