Dodoma. Serikali imeeleza haina mpango wa kubagua wanafunzi wanaotoka shule binafsi katika utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, bali inaongozwa na vigezo vya kisheria vinavyolenga kuwabaini wanafunzi wenye uhitaji halisi bila kujali walikotoka kielimu.
Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumatano, Januari 28, 2026 na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Amir Hafidh wakati akijibu swali la Devotha Mburarugaba (Viti Maalum) aliyehoji Serikali haioni umuhimu wa kurekebisha kigezo kinachowapunguzia fursa wanafunzi waliotoka shule binafsi, kupata mikopo ya vyuo vya elimu ya juu.
Akijibu swali hilo, Wanu amesema upangaji na utoaji wa mikopo ya elimu ya juu unaongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (sura ya 178), ambayo inaainisha wazi sifa za msingi za mwombaji.
Amesema miongoni mwa sifa hizo ni pamoja na kuwa na vigezo vya kitaaluma vya kujiunga na taasisi za elimu ya juu pamoja na kuthibitika kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za masomo.
“Msingi mkubwa wa utoaji wa mikopo ni uhitaji wa kiuchumi wa mwanafunzi, si aina ya shule aliyosoma,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaotoka katika kaya maskini bila kujali kama wamesoma shule za Serikali au binafsi.
“Bodi ya mikopo imeweka utaratibu unaowahusisha waombaji wote kwa usawa, mradi tu wametimiza vigezo vilivyowekwa, ikiwemo kujaza taarifa sahihi wakati wa maombi, ” amesema.