MBUNGE WA KIBAMBA ATEMBELEA VIVUKO, AGHARAMIA UJENZI NA ATOA AHADI YA SULUHISHO LA KUDUMU

Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Mheshimiwa Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ametembelea Kivuko cha Mabrouk na Kivuko cha Matembezi vilivyopo Mtaa wa Kibamba, Kata ya Kibamba, kwa lengo la kujionea hali halisi ya miundombinu ya vivuko hivyo na kubaini changamoto zinazowakabili wananchi wanaovitumia katika shughuli zao za kila siku.

Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Kairuki amesema amechukua hatua ya kugharamia kiasi cha shilingi 2,745,000 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kivuko cha Mabrouk ili kiweze kupitika kwa usalama na waenda kwa miguu.

Hatua hiyo inalenga kupunguza adha kwa wananchi pamoja na kuzuia matukio ya vifo vilivyokuwa vikijitokeza mara kwa mara, hususan nyakati za mvua kubwa ambapo baadhi ya wananchi walikuwa wakisombwa na maji.

Kwa upande wa Kivuko cha Matembezi, ambacho kimekuwa kwenye mipango kwa zaidi ya miaka 15 bila kutekelezwa, Mheshimiwa Angellah Kairuki aliwahakikishia wananchi wa Mtaa wa Kibamba kuwa atalifuatilia kwa karibu na kuhakikisha linapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuondoa changamoto hiyo ya muda mrefu.

Wananchi wa Kibamba wamepongeza jitihada za Mbunge wao, wakieleza kuwa hatua hizo zinaonesha dhamira ya dhati ya kiongozi wao katika kusikiliza, kushughulikia na kutatua changamoto za msingi zinazowagusa moja kwa moja katika maisha yao ya kila siku.