‘Vishandu’ waibua hofu Tanga, polisi wakamata watuhumiwa 55

Tanga. Vijana wanaohofiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu maarufu kama vishandu wameendelea kuwa tishio kwa usalama wa wakazi wa Jiji la Tanga, wakihusishwa na uporaji wa simu, kuvunja biashara na wizi wa vyombo vya usafiri, huku wakitumia silaha za jadi zikiwemo mapanga na nondo.

Uchunguzi wa Mwananchi uliofanywa katika mitaa mbalimbali katikati ya jiji umebainisha kuwa wananchi wengi wameathirika na vitendo hivyo, hali iliyosababisha hasara kubwa za kiuchumi na kuvuruga shughuli zao za kila siku.

Mmoja wa waathirika, Asia Radedi, mkazi wa Kisosora, alisema vijana hao walivunja saluni yake ya kusuka nywele na kuiba mali zenye thamani ya zaidi ya Sh1.5 milioni.

“Alhamisi asubuhi nilipigiwa simu na kuambiwa ofisi yangu iko wazi. Nilipofika nikakuta wamevunja na kuondoa kila kitu cha biashara,” alisema Asia.

Alisema tukio hilo limemwathiri kwa kiasi kikubwa kwani alianzisha biashara hiyo kwa mkopo ambao bado hajamaliza kuurejesha.

“Biashara hii ndiyo ilikuwa inanisaidia kulipa karo za watoto wangu. Sasa sijui nifanye nini, hata kukopa tena siwezi kwa sababu tayari nina deni,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kisosora Kusini na Diwani wa Kata ya Chumbageni, Ng’wenga Juma, alisema kundi hilo limekuwa tishio kubwa kwa usalama wa mtaa na kata nzima, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa jamii katika kudhibiti uhalifu.

“Hawa vijana wanajulikana na jamii. Si sahihi kuwaachia polisi pekee, wakati wananchi wengine wanaendelea kuwaficha,” alisema Ng’wenga.

Aliongeza kuwa vijana hao hutembea nyakati za usiku wakiwa kwenye pikipiki nne hadi tano, wakiwa na silaha, na kutumia vijiwe kama maficho yao.

Alisema kwa ushirikiano wa wananchi, baadhi ya vijiwe vimefanikiwa kudhibitiwa, ikiwemo maskani ya Maniga ambayo imepigwa marufuku.

Mkazi wa Mtaa wa Madina, Osca Asenga, alisema aliibiwa simu baada ya wahalifu hao kukata wavu wa dirisha akiwa usingizini.

“Nilishangaa kuona wavu wa dirisha umekatwa bila mimi kusikia chochote. Ninaamini walinifukizia dawa,” alisema.

Naye Rashid Abdalah, muuza chips katika Mtaa wa Ngome, alisema vijana hao huwalazimisha wafanyabiashara kuwapa chakula bila malipo.

 “Wanapofika na mapanga huwezi kukataa. Wanakula, wanachukua na kuondoka, na huwezi kutoa taarifa kwa kuogopa usalama wako,” alisema.

Akizungumzia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, alisema Serikali imechukua hatua madhubuti kwa kushirikiana na viongozi wa kata na wananchi.

“Jamii isiwaachie viongozi au polisi pekee. Wahalifu wengi wanajulikana, kinachotakiwa ni kutoa taarifa mapema,” alisema.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi, alisema operesheni maalumu zimefanikiwa kudhibiti hali hiyo.

“Katika operesheni hizo, jumla ya simu 60 zimekamatwa, ambapo simu 35 zimetambuliwa na kurejeshwa kwa wamiliki wao,” alisema ACP Mchunguzi.

Aliongeza kuwa jumla ya watuhumiwa 55 wamekamatwa kwa makosa mbalimbali, wakiwemo tisa wanaotuhumiwa kujihusisha na unyang’anyi wa kutumia silaha na wizi wa pikipiki.

Makosa mengine ni pamoja na wizi, uporaji, makosa ya usalama barabarani na makosa ya kimaadili.

Aidha, pikipiki 50 zimekamatwa, zikiwemo 28 zisizo na namba halali za usajili.

Katika operesheni hizo pia, mali mbalimbali zinazodhaniwa kuwa za wizi zimekamatwa, ikiwemo luninga saba, friji moja, magodoro matatu pamoja na madumu 26 ya mafuta ya dizeli.