JKT Tanzania imesema bado inahitaji kuongeza kasi na kujituma kusaka pointi tatu kila mechi ili kumaliza nafasi nne za juu katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Timu hiyo imeonekana kuwa moto msimu huu ikiwa imekaa kileleni mara kadhaa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ambapo kabla ya jana Yanga kucheza dhidi ya Dodoma Jiji, ilishika nafasi ya kwanza kwa pointi 21 huku ikishuka dimbani mara 12.
Kocha Mkuu wa JKT Tanzania, Ahmad Ally, amesema juhudi binafsi na wachezaji kufuata maelekezo ndio siri ya kufanya vizuri, akieleza kuwa licha ya mafanikio hayo, lakini bado ni mapema kutamba.
Amesema matokeo waliyonayo wanayatumia kama sehemu ya hamasa kikosini kuendelea kupambana kila mchezo kupata pointi tatu akieleza kuwa ushindani ni mkali na hawawezi kuridhika na walichonacho kwa sasa.
“Niwapongeze vijana wangu wanajituma wakiwa uwanjani, haya matokeo ni sehemu ya hamasa kwetu katika kuendelea kupambana kutafuta ushindi kila mchezo, malengo ni kuona tunamaliza nafasi nne za juu.
“Tunapata ushirikiano kutoka kwenye uongozi hali inayoongeza ari, morali na nguvu kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake, ni mapema kutamba kwakuwa ligi haijaisha na timu zinaonesha ushindani,” amesema kocha huyo.
Amesema baada ya kukosa pointi tatu katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons wakitoka 0-0, wanaenda kusahihisha makosa haswa eneo la ushambuliaji kuhakikisha wanapata ushindi na kufunga mabao katika mchezo ujao dhidi ya Dodoma Jiji utakaochezwa Januari 29 mwaka huu.
Kwa upande mshambuliaji wa timu hiyo, Valentino Mashaka, amesema siri ya mafanikio kwake na timu kwa ujumla ni kufanya kazi kwa ushirikiano na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi akieleza kuwa mkakati wao ni kuendelea kupambana ndani ya uwanja.
“Ninachoamini ni kujituma na kufuata maelekezo ya kocha, tunacheza kwa ushirikiano na hatuwezi kubweteka kwa matokeo haya kwakuwa ni mapema ligi haijaisha, niwaombe mashabiki wazidi kutusapoti,” amesema nyota huyo anayecheza hapo kwa mkopo akitokea Simba.