KIPIGO cha mabao 6-0 dhidi ya Yanga ugenini, bado kinaendelea kulitesa benchi la ufundi la Mashujaa FC baada ya kocha mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga kufichua kwamba walifanya makosa ambayo bado yanamsumbua kuyatatua kabla ya kukutana na mpinzani mwingine.
Januari 19, 2026, timu hiyo kutoka Kigoma iliambulia kipigo cha mabao 6-0 kutoka kwa Yanga kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Hii imekuwa ni kama mazoea kwa Yanga kuishushia Mashujaa kipigo kikali kwani msimu uliopita iliichapa 5-0 nyumbani kwao Kigoma.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga amesema waliingia kwenye mchezo huo na mipango mizuri ya kuiheshimu Yanga lakini bao la mapema dakika ya nane lilitibua kila kitu na kuwachanganya wachezaji.
“Matokeo hayo nimeyapokea, lakini yalilivuruga benchi na wachezaji kwa ujumla kwani ni kipigo kikubwa ambacho hatukukitarajia. Hatuwezi kurudia makosa haya kwani tayari nimeanza kufanyia kazi upungufu uliotugharimu.
“Ni kweli tulikutana na mpinzani bora, lakini hatukustahili matokeo haya kama tusingefanya makosa, naamini wachezaji wangu pia waliumizwa na matokeo yale, hivyo hawatakubali kurudia makosa kama waliyofanya kuelekea mechi zijazo,” amesema Mayanga.
Mayanga amesema wamekutana na Yanga mara nyingi na kufanikiwa kudhibiti ubora wao lakini mchezo uliopita walizidiwa na kujikuta wakiruhusu mabao mengi.
Amesema wametambua makosa na kuyafanyia kazi licha ya kwamba haikuwa rahisi kutokana na saikolojia ya wachezaji wake kutokuwa sawa.
“Haikuwa rahisi kusawazisha makosa kwani wachezaji pia hawakuwa katika hali nzuri kwani kipigo kilikuwa ni kikubwa, hawakukitarajia lakini kama benchi la ufundi tumefanya kazi ya ziada kuhakikisha tunawajenga wachezaji na wanarudi kwenye mstari wa ushindani,” amesema