Dar es Salaam. Katika juhudi za kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa anga barani Afrika, Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limezindua rasmi safari za moja kwa moja kwenda Accra, Ghana kupitia Lagos, Nigeria ikilenga kukuza utalii, kuimarisha uchumi na kurahisisha usafiri kati ya Afrika Mashariki na Magharibi.
Safari za Accra zitakuwa mara tatu kwa wiki Jumatatu, Jumatano na Ijumaa itaondoka changamoto ya awali ambapo wasafiri kutoka Tanzania walilazimika kutumia mashirika ya ndege ya nje na kupitia nchi kama Ethiopia, Dubai, Istanbul au Qatar kufika mataifa ya Afrika Magharibi kama Ghana, Senegal na Ivory Coast.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa safari hiyo iliyofanyika Dar es Salaam leo Jumatano, Januari 28, 2026, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa habu ya usafiri wa anga, kwa kuunganisha abiria kutoka Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani.
“Awali abiria walilazimika kupitia Nairobi na kusubiri kwa muda mrefu, lakini sasa Air Tanzania itafanya safari za moja kwa moja kupitia Lagos hadi Accra. Hii ni hatua ya kimkakati itakayorahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kati ya mataifa haya,” amesema Profesa Mbarawa.
Amesema safari hizo zitasaidia kuimarisha uhusiano wa kihistoria, kiutamaduni na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi za Afrika Magharibi na zitachochea ongezeko la watalii, uwekezaji na biashara.
“Watu wengi wa Afrika Magharibi wanaufahamu utalii wa Zanzibar. Kupitia safari hizi za moja kwa moja, watapata fursa rahisi ya kufika Dar es Salaam na Zanzibar,” amesema.
Profesa Mbarawa amesema kutokana na mahitaji ya soko, Serikali ina mpango wa kuanzisha safari za moja kwa moja kutoka Zanzibar kwenda Afrika Magharibi siku za usoni.
“Uzinduzi huu unaweka Tanzania kama kiunganisho muhimu kati ya Afrika Mashariki na Magharibi, na kufungua fursa kwa wafanyabiashara, wawekezaji na wasafiri,” amesema.
Amesema Serikali inatarajia kuona ongezeko la watalii na wawekezaji kutoka Afrika Magharibi, huku akihimiza Watanzania, hususan wajasiriamali, kutumia fursa hiyo kujenga ushirikiano wa kibiashara.
“Watalii watatembelea Mlima Kilimanjaro, Zanzibar na vivutio vingine. Hili ni daraja muhimu la kiuchumi na lazima tulitumie ipasavyo,” amesema.
Profesa Mbarawa amesema safari hizo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha Shirika la Ndege Tanzania kama rasilimali ya kimkakati na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa anga.
“Tunataka abiria kutoka Afrika Magharibi watumie Tanzania kama kiunganisho kwenda India na China. Safari kutoka Afrika Magharibi hadi Tanzania ni takribani saa tano, na kutoka hapa hadi India au China ni saa tano nyingine jumla ya saa 10 pekee,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Air Tanzania, Peter Ulanga, amesema safari za ndege kwenda Accra, Ghana ni ndoto ya muda mrefu iliyotimia na itatoa fursa kwa mashabiki wa soka kusafiri na kuziunga mkono timu zao katika michuano ya Afcon ijayo.
Amesema shirika hilo limeendelea kukua kutoka kuwa na ndege tisa mwaka 2021 hadi kufikia ndege 16 kwa sasa, huku vituo vya safari vikiongezeka kutoka 24 hadi 32 ndani ya miezi 15.
Amesema vituo vya kimataifa vilivyoongezwa ni pamoja na Cape Town, Zimbabwe, Kinshasa, Lagos na Accra, huku ndani ya nchi zikirejeshwa safari za Pemba, Mtwara na Iringa.
Ulanga amesema idadi ya abiria imeongezeka kutoka 500,000 mwaka 2020/2021 hadi kufikia milioni 1.5 mwaka jana, sawa na ongezeko la asilimia 200, na kwa sasa shirika lina wafanyakazi wapatao 1,000.
Safari za Accra zitakuwa mara tatu kwa wiki Jumatatu, Jumatano na Ijumaa kwa kutumia ndege yenye uwezo wa kubeba abiria 180, huku matarajio yakiwa ni kusafirisha abiria 4,000 kwa mwezi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, amesema mwaka 2016 alilikuta Shirika la Ndege hilo likiwa katika hali mbaya kiuchumi ikilinganishwa na sasa mwaka 2026 alipokuwa anachukua uongozi wa Kamati hiyo.
“Nililikuta Shirika la Ndege likiwa na ndege moja pekee na wafanyakazi zaidi ya 200 waliokuwa wakitegemea ndege hiyo moja,” amesema Kakoso.
Amesema hali hiyo imebadilika ambapo sasa shirika linajiendesha kibiashara na kuwalipa watumishi wake kwa kutumia mapato ya ndani bila kutegemea Serikali.
“Si rahisi kutoka kwenye ndege moja hadi kufikisha 16 leo fursa zimeongezeka ikiwemo safari za moja kwa moja Afrika Magharibi,” ameongeza.
Pia Kakoso amelitaka Shirika hilo kuongeza ndege kwani mahitaji ndani ya nchi ni makubwa ndiyo maana zimekuwa zikijaa na wengine wakihangaika kusaka usafiri.
“Tunahitaji kuwa na ndege za kutosha kurahisisha usafiri, Watanzania wengi sasa hawataki kusafiri kwa mabasi wanataka ndege,” amesema.