Mwingine afariki ajali ya basi na lori Tinde 

Shinyanga. Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (Mwawaza), Dk Jonathan Chikomele, amethibitisha kifo cha mtu mwingine mmoja aliyejeruhiwa katika ajali ya basi na lori iliyotokea katika eneo la Mnada wa Tinde.

Akizungumza na mwandishi wa habari kwa njia ya simu leo Januari 28, 2026, Dk Chikomele amesema marehemu ametambuliwa kwa jina la Jackson Abbubakar (38), ambaye alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu hospitalini hapo.

“Tumempokea Jackson Abbubakar akiwa katika hali mbaya. Baada ya kumfanyia vipimo, ilibainika kuwa bandama lake limepasuka. Madaktari walifanya juhudi zote za haraka kumuokoa, lakini hatukufanikiwa na alifariki dunia,” amesema Dk Chikomele.

Katika picha ni roli kilikuwa limebeba mchele kutoka Rwanda lililopata ajali lenye namba za usajili RAE 849 N.



Ameongeza kuwa hospitali hiyo ilipokea jumla ya majeruhi tisa kutoka katika ajali hiyo, ambapo sita waliruhusiwa baada ya kupata matibabu, huku wengine wawili wakiendelea na matibabu.

“Wagonjwa wawili waliobaki wanaendelea vizuri na matarajio ni kuwa wataruhusiwa baada ya siku mbili au tatu kulingana na hali zao,” ameongeza.

Ajali hiyo ilitokea Januari 27, 2026 ikihusisha basi la kampuni ya Kisire, lililokuwa likisafiri kutoka Kahama kwenda Mwanza, na lori kutoka nchini Rwanda, lililokuwa limebeba shehena ya mchele.

Katika ajali hiyo, dereva wa lori hilo, Hitayezu Elias (35), alifariki dunia papo hapo.

Katika picha ni roli kilikuwa limebeba mchele kutoka Rwanda lililopata ajali lenye namba za usajili RAE 849 N.



Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, alisema ajali ilitokana na mwendo kasi wa basi hilo.

Magomi alisema basi lilipofika katika eneo la Mnada wa Tinde liligonga toroli la matikiti kabla ya kugongana uso kwa uso na lori hilo.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo huku likiwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika.