Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, amesema wazi kuwa hajawasiliana na mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff katika siku za hivi karibuni wala kuomba kufanyika kwa mazungumzo yoyote na Washington.
Akizungumza na vyombo vya habari vya serikali, Araghchi alikanusha madai yaliyotolewa na Rais wa Marekani Donald Trump, akisisitiza kuwa msimamo wa Iran kuhusu mazungumzo bado haujabadilika.
Kauli hiyo imekuja wakati mvutano kati ya Tehran na Washington ukiendelea kuongezeka, hasa baada ya Trump kusema kuwa “armada” nyingine ya kijeshi ya Marekani iko njiani kuelekea Iran.
Trump alisema anatumaini Iran itachagua kufanya makubaliano na Marekani, lakini kwa upande wa Tehran, kauli hiyo imeonekana kama shinikizo na tishio la kijeshi badala ya mwaliko wa kidiplomasia.
Araghchi alieleza kuwa, ingawa hakujakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na Marekani, bado kuna wapatanishi mbalimbali wa kikanda na kimataifa wanaoendelea kufanya mashauriano na kuwa katika mawasiliano na Iran.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa mawasiliano hayo hayawezi kuchukuliwa kama mazungumzo rasmi, na kwamba Iran haitakubali kuketi mezani wakati bado inakabiliwa na vitisho na masharti makubwa kutoka Washington.
🔴 Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.
Related
