Dodoma. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imezindua mfumo wa huduma kidijitali kwa wateja unaotumia akili mnemba (AI), ujulikanao kama Bwanaboom na Bibiboom, kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa taarifa na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu.
Mfumo huo umeunganishwa moja kwa moja na mifumo ya ndani ya mikopo ya HESLB na unatoa majibu ya papo kwa papo kwa walengwa, hatua inayotarajiwa kupunguza safari zisizo za lazima, foleni ndefu na wingi wa malalamiko kutoka kwa wanafunzi na wazazi.
Akizungumza leo Januari 28, 2026 wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) wa HESLB, Bahati Singa, amesema kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo, bodi ilikuwa na uwezo wa kuwahudumia walengwa kati ya 5,000 hadi 6,000 kwa wakati mmoja, lakini sasa imeongeza uwezo huo hadi zaidi ya walengwa 10,000.
“Kadri matumizi ya mfumo yanavyoongezeka, tunatarajia kuwahudumia kati ya walengwa 100,000 hadi 200,000 kwa wakati mmoja.
“Mfumo wa Bwanaboom na Bibiboom umeunganishwa moja kwa moja na taarifa za mikopo, hivyo mteja anauliza swali na kupata jibu papo hapo bila kusubiri siku kadhaa au kufika ofisini,” amesema Singa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Bill Kiwia, amesema kuanzishwa kwa mfumo huo ni sehemu ya mkakati wa bodi wa kutumia teknolojia kuboresha huduma kwa wateja.
“Awali, tulikuwa na changamoto kubwa ya kuwafikia walengwa wengi kwa wakati mmoja kutokana na wingi wa maswali na maombi. Mfumo huu utapunguza malalamiko, kuongeza ufanisi na kuharakisha huduma kwa wanafunzi na wazazi,” amesema Kiwia.
Ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yatapunguza mzigo kwa wafanyakazi na kuwawezesha kujikita zaidi katika kazi za kimkakati na za kitaalamu.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, amesema mfumo huo unatarajiwa kupunguza gharama za utoaji wa huduma za mikopo kwa takribani asilimia 60, huku ukihakikisha uwazi na uwajibikaji.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi
“Hatupaswi kuendelea kuwa watazamaji wa teknolojia zinazobuniwa. Ni hatua ya kujivunia kuona Bodi ya Mikopo ikianzisha mfumo wake wa kidijitali. Nawahimiza Watanzania kuutumia kikamilifu,” amesema Profesa Mushi.
Uzinduzi wa mfumo huo umepokelewa kwa mtazamo chanya na baadhi ya wanafunzi na wazazi, ambao wamesema utapunguza gharama na usumbufu waliokuwa wakikumbana nao awali.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Backline Humbaro, amesema chatbot hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi walioko mbali na ofisi za HESLB.
“Mara nyingi tulikuwa tunasafiri umbali mrefu kuuliza maswali madogo tu. Mfumo huu utapunguza gharama, muda na msongo wa mawazo,” alisema.
Hata hivyo, ameshauri HESLB kuhakikisha mfumo huo unalinda usiri wa taarifa binafsi za watumiaji, hauwabagui walengwa na unazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.