Upungufu wa madawati 6,290 wachangia msongamano wa wanafunzi Tabora Manispaa

Tabora. Halmashauri ya Manispaa ya Tabora inakabiliwa na upungufu wa madawati 6,290 kwa shule za msingi pamoja na sekondari hali inayosababisha msongamano wa wanafunzi katika dawati moja.

Hali hiyo inatajwa kuondoa utulivu wa mwanafunzi pindi mwalimu anapofundisha ikiwa ni pamoja na kushindwa kuandika vizuri kutokana na kukaa watoto zaidi ya wanne kwenye dawati moja.

Hayo yamebainishwa leo Januari 28, 2026 na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, John Pima wakati akizungumza na Mwananchi juu ya changamoto ya madawati manispaa ya Tabora ikizingatiwa shule zimefunguliwa na tayari wanafunzi wameanza masomo.

“Manispaa yetu wanafunzi wanaongezeka kila wakati sasa na sisi hatuwezi kusema watoto wasisome wakati Rais anawekeza fedha nyingi kwa ajili yao, sasa tunachofanya ni kuendelea kutengeneza madawati ili watoto wakae,” amesema.

Amesema awali halmashauri ilikua imetenga Sh370 milioni kwa ajili ya kutengeneza madawati lakini manispaa ikafanikiwa kupokea magogo pamoja na mbao kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Wilaya ya Tabora kwa ajili ya kutengeneza madawati kwa shule za msingi na sekondari.

Aidha amesema bajeti ya sasa ni jumla ya Sh148 milioni kwa ajili ya utengenezaji huo wa madawati ambapo amesema yatatengenezwa madawati 1,500 kwa shule za msingi na madawati 1,000 kwa shule za sekondari za Manispaa ya Tabora.

“Kwa kupata magogo haya na fedha tulizoandaa basi tutachonga madawati ili tuwapunguzie adha watoto wetu kama sio kuondoa kabisa na naamini kutatuliwa kwa changamoto hii kutachagiza hata ongezeko la ufaulu,” amesema.

Mwanafunzi wa darasa la tano Jamila Mpanzu, amesema wanafunzi wanachafuka kwa sababu muda mwingine wanaona bora hata kukaa chini kuliko wanavyosongamana kwenye dawati hawaandiki vizuri, hivyo kuiomba Serikali ione umuhimu wa kuharakisha shughuli ya uchongaji madawati.

Juma Bakari ambaye pia ni mwanafunzi manispaa ya Tabora amesema uwezo wa darasani wanao kwa sababu kuna utaratibu wa chakula shuleni, ila changamoto kubwa ni upungufu wa madawati hivyo kukosa utulivu wakati mwalimu anafundisha.

Kwa sasa bado kuna wanafunzi kadhaa wako majumbani hawajaripoti shuleni kwa darasa la kwanza na kidato cha kwanza pia, haifahamiki kwamba endapo watawasili shuleni kwa wakati huu watakaa wapi.