Tiseza yahamasisha uwekezaji wa ndani, yakagua maeneo ya kongani za viwanda

Simiyu. Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) imeanza kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, sambamba na ukaguzi wa maeneo maalumu yaliyotengwa kwa ajili ya uanzishaji wa kongani za viwanda nchini.

Imeelezwa kuwa kampeni hiyo inalenga kuyafikia makundi mbalimbali yakiwemo vijana wajasiriamali wadogo na wa kati, wafanyabiashara, waandishi wa habari pamoja na maofisa wanaosimamia sekta za viwanda, biashara na uwekezaji kutoka sekretarieti za mikoa na halmashauri kote nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Januari 27, 2025 mkoani Simiyu, Mwenyekiti wa Bodi ya Tiseza, Balozi Dk Aziz Mlima, amesema mamlaka hiyo imejipanga kutoa vivutio mbalimbali kwa wawekezaji wa ndani, ikiwemo misamaha ya kodi kwa wawekezaji wanaosajiliwa chini ya mamlaka hiyo, ili kuwasaidia kukuza mitaji yao.

Mlima amesema kampeni hiyo inalenga kubadili fikra iliyojengeka kwa muda mrefu miongoni mwa Watanzania kwamba uwekezaji ni kwa ajili ya wageni pekee, huku akisisitiza kuwa wazawa wana uwezo mkubwa wa kuwekeza endapo watapatiwa elimu sahihi na mazingira rafiki.

“Tunatoa elimu ya uwekezaji kwa lengo la kujenga hamasa na kuongeza idadi ya wawekezaji wa ndani. Watanzania wanahamasishwa kuwekeza katika sekta zitakazozalisha ajira na fursa za kiuchumi, badala ya kutumia fedha nyingi za kigeni kuagiza bidhaa kutoka nje,” alisema Dk Mlima.

Ameongeza kuwa kila mkoa una fursa zake za kipekee, akitaja Mkoa wa Simiyu kuwa na uwezekano mkubwa wa uwekezaji katika viwanda vya kuchakata pamba, minofu ya samaki, maziwa na nyama.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anamringi Macha, amesema mkoa huo ambao ni kinara wa uzalishaji wa pamba ulikuwa unakabiliwa na changamoto ya uhaba wa umeme, lakini Serikali imechukua hatua kwa kujenga kituo cha kupozea umeme kinachotarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.

Naye Meneja Masoko na Manunuzi wa Kiwanda cha Moli Co. Ltd cha mjini Bariadi, Alphat Ally amesema mazingira ya uwekezaji nchini kwa sasa ni rafiki, huku kukiwa na uwezeshaji mkubwa kutoka serikalini.

Sehemu ya mitambo ya kiwanda cha kutengeneza mabomba cha Moli Co Ltd cha mjini Bariadi kilichotembelewa na wajumbe kutoka TISEZA. Picha na Samwel Mwanga



Amesema kampuni hiyo imeamua kuwekeza mkoani Simiyu kwa kuzingatia kuwa ni kuwekeza nyumbani, sambamba na kutoa ajira kwa Watanzania, huku bidhaa zake zikisambazwa katika Kanda ya Ziwa, Kati na Magharibi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji wa Tiseza, George Mukono, amesema mwekezaji wa Moli Co. Ltd alipata usaidizi mkubwa kutoka mamlaka hiyo, ikiwemo misamaha ya kodi na msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), hali iliyochangia kufanikiwa kwa uwekezaji huo.

Katibu Tawala Msaidizi anayesimamia viwanda, biashara na uwekezaji Mkoa wa Simiyu, Porches Tumaini, amesema mkoa huo tayari umetenga maeneo maalumu kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda, huku akiwahimiza wawekezaji wa ndani kujitokeza kuchangamkia fursa hizo.

Mkazi wa Bariadi, Hassan Mohamed, amesema elimu ya uwekezaji ni muhimu kwa Watanzania wengi ambao bado wana hofu ya kuanzisha viwanda.

“Wengi wetu tunadhani kuanzisha kiwanda ni gharama kubwa sana, lakini tukipata elimu na vivutio kama misamaha ya kodi, tunaweza kuanza hata kwa kiwango cha kati,” amesema.

Naye Rehema Butondo, mjasiriamali wa bidhaa za maziwa mjini Bariadi, amesema uwepo wa Tiseza mkoani humo ni fursa kwa wazalishaji wadogo.

“Tunazalisha maziwa mengi lakini viwanda vya kuchakata ni vichache. Kama Serikali inahamasisha uanzishaji wa viwanda, sisi wafugaji tutafaidika moja kwa moja,” amesema.