Manispaa ya Morogoro yaanza kuwaondoa wafanyabiashara barabarani

Morogoro. Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro imeanza operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara wanaofanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi, ikiwemo kando ya barabara, kufuatia ongezeko la wafanyabiashara wa mboga na matunda wanaovamia maeneo hayo.

Akizungumza na Mwananchi leo Januari 28, Ofisa Habari wa Manispaa ya Morogoro, Lilian Heneriko, amesema operesheni hiyo ilianza Januari 26, 2026 na inatekelezwa kwa kushirikiana na askari wa Jeshi la Akiba (mgambo).

Amesema lengo ni kuwalazimisha wafanyabiashara kurejea katika masoko rasmi yaliyopo ndani ya manispaa badala ya kufanya biashara barabarani au maeneo yasiyoruhusiwa.

“Tunawaomba wafanyabiashara wazingatie sheria na taratibu. Masoko yapo na wateja watawafuata huko,” amesema Heneriko.

Ameongeza kuwa tangu operesheni kuanza, baadhi ya wafanyabiashara wameitikia na kurejea sokoni, ingawa wapo wanaoendelea kufanya biashara kwa kificho.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Chifu, Khalid Mkunyegele, amesema biashara sokoni imeathirika kutokana na wateja wengi kununua bidhaa barabarani.

“Tatizo ni kuwa wafanyabiashara wanapoondolewa hurudi tena baada ya muda mfupi, jambo linalowaumiza waliobaki sokoni,” amesema, akionya kuwa masoko rasmi yanaweza kubaki matupu endapo hatua za kudumu hazitachukuliwa.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara wa barabarani wamesema wanachochewa na changamoto za upatikanaji wa wateja katika masoko rasmi.

Shida Salumu, mfanyabiashara wa mboga na matunda katika Barabara ya Madaraka, amesema Soko la Chifu Kingalu lina changamoto za miundombinu.

“Eneo la kuuzia mbogamboga lipo ghorofani, hali inayowakatisha tamaa wateja wengi,” amesema, akiongeza kuwa maeneo yenye mkusanyiko mkubwa wa watu kama vituo vya mabasi huvutia zaidi biashara.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wakazi wa Morogoro wamelalamikia wafanyabiashara hao wakidai wanachangia msongamano na uchafuzi wa mazingira. Mkazi wa Morogoro, Aziz Habibu, ameishauri Manispaa kutenga maeneo maalumu yenye miundombinu rafiki kwa wafanyabiashara wadogo.

“Kuwaondoa pekee hakutoshi, ni muhimu kupanga maeneo rasmi yatakayowafaidi wafanyabiashara na mji kwa ujumla,” amesema.