Wakili Madeleka aibuka kidedea kortini, ombi la Jamhuri lakataliwa

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imelikataa ombi la upande wa Jamhuri la kutaka kuifanyia marekebisho hati ya mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi baada ya Mahakama kulikubali pingamizi la wakili Peter Madeleka.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkuu Mkazi, Gwantwa Mwankuga wakati akitoa uamuzi shauri la uhujumu uchumi namba 5195 la 2025 baada ya Jamhuri kuomba kuifanyia marekebisho hati katika hatua ya ukabidhi.

Kesi hiyo ya uhujumu uchumi ambayo Mahakama Kuu Divisheni ya makosa ya Rushwa na Uhujumu uchumi ndio yenye mamlaka ya kuisikiliza, inawakabili washtakiwa saba ambao ni pamoja na Joseph Matage na Grace Matage.

Washtakiwa wengine katika shauri hilo ambalo limehamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi ni Jamaal Saad, Mubinkhan Dalwai, Stanley Tibehendra, Edward Ochieng’ Omeno na Bushra Juma Ali.

Wanakabiliwa na makosa tofauti tofauti 52 yanayohusu kuongoza genge la uhalifu, kughushi nyaraka, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji fedha zaidi ya dola milioni 5.1 za Marekani.

Fedha hizo ni karibu Sh13 bilioni za Tanzania, na upande wa Jamhuri unadai makosa hayo yalitendeka kwa tarehe tofauti tofauti kati ya Januari 1,2024 na Novemba 30 katika Jiji la Dar es Salaam.

Pingamizi la Madeleka lilivyokuwa

Katika pingamizi lake, Wakili Madeleka anayemtetea mshtakiwa wa tatu, Saad, alijenga hoja kuwa ingawa sheria inaruhusu kurekebishwa kwa hati ya mashtaka, uwezo huo unaweza kutumika tu katika hatua yoyote ya kesi wakati wa usikilizaji.

Kwa mujibu wa Wakili Madeleka, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu si mahakama ya kusikiliza kesi (trial court) na shauri hilo lipo mbele ya mahakama hiyo kwa madhumuni ya mwenendo kabidhi.

Aliendelea kueleza kuwa washtakiwa bado hawajatakiwa kukiri au kukanusha mashitaka (plea taking) kwa hivyo kifungu cha 251(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023 hakitumiki.

Alieleza kuwa ikiwa upande wa mashtaka ungependa kurekebisha dosari yoyote, hatua sahihi itakuwa ni kuondoa shauri mahakamani au kuingiza kusudio la kusitisha mashitaka (nolle prosequi) kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).

Ukijibu hoja hizo, upande wa mashitaka ulikubali kuwa hiyo si mahakama inayosikiliza shauri hilo lakini ukasema mahakama lazima ielewe vizuri shtaka hilo na washtakiwa wote lazima wawepo mahakamani ipasavyo, ili mwenendo wa kuhamishia kesi Mahakama Kuu (committal proceedings) uendelee kisheria.

Upande wa mashitaka ulitegemea uamuzi wa Mahakama ya Rufaa katika shauri la Jamhuri dhidi ya Farid Ally Ahmed na wengine. Rufaa ya Jinai namba 59 ya 2015, ukieleza kuwa mahakama ya chini inayoshughulikia hatua za kuhamisha shauri kwenda Mahakama Kuu ina mamlaka ya kuamuru kukamatwa au kuletwa kwa mshtakiwa na kusomewa maelezo ya mashtaka kabla ya kuhamishwa.

Hata hivyo, upande wa utetezi, katika majibu yao ya hoja za ziada, walisisitiza kuwa mamlaka yaliyotajwa hayaiwezeshi Mahakama hiyo kurekebisha shitaka katika hatua ya ukabidhi na Mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria.

Katika uamuzi wake alioutoa Januari 26,2026 na nakala yake kupatikana Januari 28,2026, Hakimu Mwankuga alisema hoja ambayo mahakama inapaswa kuamua iwapo katika hatua ya ukabidhi, mahakama inaweza kulikubali ombi la Jamhuri.

Alisema maudhui ya kifungu 251 cha CPA kiko wazi kuwa mahakama hiyo sio inayosikiliza shauri hilo na katika hatua hiyo, washtakiwa bado hawajatakiwa kujibu lolote kuhusiana na mashitaka ya uhujumu uchumi yanayowakabili.

“Kwa hivyo, ombi lolote la kutaka kurekebisha hati ya mashitaka limekuja mapema kabla ya wakati kwa kuwa marekebisho itaonekana kama imefanyika wakati wa usikilizwaji kwani usikilizaji unaanza anapokuwa kwenye mahakama yenye uwezo wa kusikiliza shauri husika.”

Hakimu alisema Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kama mahakama ya ukabidhi ambayo jukumu lake la msingi ni kupima kama ushahidi wa kutosha kuhamishia kesi mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza ambayo ni Mahakama Kuu.

“Mahakama haiwezi kuruhusu marekebisho ya msingi ya shtaka ambayo yataathiri haki za mshtakiwa au kwenda kinyume na taratibu zilizowekwa,”alisema.

Akirejea msimamo uliotolewa katika kesi ya Jamhuri dhidi ya Mussa Ally (1989), Mahakama ya Rufani Tanzania ilisisitiza waziwazi kwamba hakimu katika hatua ya ukabidhi, hana mamlaka ya kubadilisha au kurekebisha hati ya mashitaka.

“Jukumu la mahakama hii  limejikita kikamilifu katika kuamua ikiwa kuna ushahidi wa awali (prima facie case) wa kuhalalisha kumfikisha mtuhumiwa Mahakama Kuu,”alisema Hakimu Mwankuga katika uamuzi wake huo na kuongeza;-

“Hivyo basi, inafuata kwamba, hakuna marekebisho wala mabadiliko ya shtaka yanayoruhusiwa katika hatua ya kuwasilisha shauri mahakama kuu (committal stage), na jaribio lolote la kufanya hivyo litakuwa nje ya uwezo wa hakimu.”

“Ingawa ni kweli, kama ilivyowasilishwa na upande wa mashitaka, kwamba Mahakama lazima ielewe shtaka na kwamba mtu anayeshtakiwa lazima awepo mahakamani ipasavyo ili hatua za awali za mashauri ziendelee, kuzingatia huko hakuipi Mahakama hii mamlaka ya kurekebisha hati ya mashitaka.”

“Hofu iliyotolewa na upande wa utetezi kwamba marekebisho katika hatua hii yanaweza kusababisha dhuluma kwa mshtakiwa, kwa hivyo, si jambo lisilo na msingi. Msingi wa mashtaka ya jinai ni hati ya mashitaka, na mabadiliko yoyote kwake lazima yafanywe kwa kuzingatia kikamilifu sheria na mahakama yenye mamlaka ya kufanya hivyo,”alisema Hakimu katika uamuzi wake.

Hakimu alisema Mahakama yake inaongozwa na kanuni iliyoelezwa katika shauri la Jamhuri dhidi ya Hamis Omary ambalo ni shauri na marejeo namba 12 la 2004.

Kwa mujibu wa Hakimu, katika shauri hilo, Mahakama iliweka msimamo kuwa haiwezi kutumia madaraka ambayo haijapewa kisheria, na tendo lolote lililofanywa bila kuwa na mamlaka ni batili.

“Hakuna kipengele cha sheria kinachoipa mahakama ya ukabidhi, uwezo wa kurekebisha hati ya mashitaka. Ni kwa msingi huo ombi la upande wa mashitaka la kufanya marekebisho hati ya mashitaka katika hatua hii linatupwa,”alisema.

Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka ulitoa orodha ya mashahidi 36 wa Jamhuri na pia itawasilisha vielelezo 121 ambavyo ni nyaraka na vielelezo halisi 9 ambavyo ni pamoja na simu za kiganjani (smartphone) 8 na flash disk 1 na DvD 1.