Dar es Salaam. Kabidhi Wasii Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Frank Frank, kupitia taarifa kwa umma, ametoa wito kwa wadai na wadaiwa wa Kampuni ya Pride kuwasilisha uthibitisho wa madai yao, huku wote wanaoshikilia mali za kampuni hiyo walipe madeni yanayowahusu na kuzikabidhi mali hizo kwa mfilisi ndani ya siku 14 kuanzia Januari 26, 2026.
Katika taarifa yake, Kabidhi Wasii Mkuu ameeleza kuwa Novemba 7, 2025, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha ilimteua kuwa mfilisi wa kampuni hiyo kupitia maombi namba 2272 ya mwaka 2025.
Frank amesema Kampuni ya Pride, iliyoanzishwa Mei 1993 kwa kuzingatia Sheria ya Kampuni Sura ya 212 kwa lengo la kutoa mikopo, na iliyokuwa na ofisi katika maeneo mengi nchini, Juni 9, 2023 Serikali ilieleza bungeni kuwa tathmini iliyofanyika nchi nzima ilitaka wote wanaodai kampuni hiyo walipwe baada ya taratibu za ufilisi kukamilika.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha wa wakati huo, Hamad Chande, amesema tathmini ya hali ya Kampuni ya Pride na ukaguzi maalumu uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu kutambua mali na madeni ya kampuni hiyo ulifanyika, akiagiza taratibu za kisheria kukamilika ili kuwezesha malipo hayo.
Chande amesema Serikali ilikuwa inaendelea na taratibu za kisheria za kuifilisi Kampuni ya Pride, na kwamba madeni yangelipwa kwa kuzingatia sheria na taratibu za ufilisi kwa mujibu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).
Ufilisi ni utaratibu wa kisheria unaomwezesha mtu au kampuni ambayo imefilisika kumalizana na wadai wake kwa mali zake kuwekwa chini ya usimamizi wa mfilisi atakayeziuza na kulipa madeni yote au sehemu yake, kama kiasi kinachopatikana hakitoshi, kama inavyoelezwa katika Sheria ya Ufilisi Sura ya 25 ya Sheria za Tanzania Bara na Sheria ya Makampuni Sura ya 212 na kanuni zake.
Pride, ambayo ni ufupisho wa maneno ya Kiingereza Promotion of Rural Initiatives and Development Enterprises, ni kampuni iliyoanzishwa Mei 5, 1993, chini ya Sheria ya Kampuni (CAP 212), kwa lengo la kutoa mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali.
Hata hivyo, taasisi hiyo ilianza kuyumba kuanzia mwaka 2016, hali iliyosababisha kushuka kwa utendaji wake siku hadi siku na hatimaye kushindwa kutoa mikopo kwa wateja wake na kulipa stahiki za wafanyakazi, ikiwemo michango ya pensheni na kodi ya Serikali.
Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Pride, iliyokuwa na makao yake makuu jijini Arusha, Rashid Malima, alipoulizwa na Mwananchi wakati huo kuhusu hali ya kifedha ya taasisi hiyo baada ya kuanza kuanguka, alisita kuzungumza akisema ametingwa na mambo mengi.
Hata hivyo, taarifa kutoka kwa baadhi ya wafanyakazi zilieleza kuwa tangu Desemba 2016, uongozi wa Pride ulianza kushindwa kuwasilisha michango ya pensheni kwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), iliyokuwa imefikia Sh1.8 bilioni, jambo lililosababisha wafungue kesi mahakamani.
Pride kushtakiwa mahakamani
Wito wa Kabidhi Wasii Mkuu hauanzishi jambo jipya, bali ni utekelezaji wa jambo lenye msingi wa kisheria na historia ndefu ya mgogoro na maamuzi ya kisheria mahakamani.
Hii ni baada ya Kampuni ya Pride kushindwa kuendelea na huduma zake, ikiwemo kurejesha mali za watu waliokuwa wakidai, na hatimaye ikashtakiwa mahakamani na kuamriwa ifilisishwe (ifungwe rasmi) baada ya kushindwa kuendelea na shughuli zake za kifedha.
Uamuzi huo ulifikiwa katika hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania (Kitengo cha Biashara) katika kesi ya Misc. Commercial Cause No. 2 of 2023, iliyohusu ombi la Serikali kupitia Msajili wa Hazina na Mwanasheria Mkuu kutaka kampuni ya Pride Tanzania Limited ivunjwe kwa sababu ya kushindwa kulipa madeni yake.
Kufuatia ripoti ya CAG ya mwaka 2019 iliyoonesha kampuni hiyo kuwa na mali za takribani Sh19 bilioni dhidi ya madeni ya zaidi ya Sh130 bilioni, wafanyakazi 234, CRDB Bank na Alliance Life Assurance waliidai malipo ya mishahara na madeni, wakitaka Serikali kama mmiliki mpya kulipa kwanza kabla ya kufungwa kwa Kampuni ya Pride.
Mahakama ilibainisha kuwa hoja kuu ilikuwa uhalali wa uamuzi wa bodi ya wakurugenzi na ushahidi wa kushindwa kulipa madeni, hivyo ikakubaliana na hoja za Serikali kwamba kampuni imefilisika na kutoa amri ya kufungwa kwa Pride Tanzania Limited, huku wadai na wadaiwa wakielekezwa kuwasilisha madai yao kwa msimamizi wa ufilisi (Rita) kwa malipo kwa mujibu wa sheria.