:::::::
Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Mhe. Anne Kilango, amempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2025.
Amesema ushindi huo wa kishindo katika Jimbo la Same Mashariki umetokana na utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia.
Akizungumza bungeni, Mhe. Kilango alimweleza Mheshimiwa Naibu Spika kuwa Mheshimiwa Rais anaongoza taifa kubwa na lenye ushawishi mkubwa ndani ya Afrika Mashariki. Alibainisha kuwa kwa kuzingatia ukubwa wa eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, bado hakuna nchi nyingi za Afrika Mashariki zinazoweza kulingana nalo, jambo linaloonesha dhamira, uwezo na juhudi kubwa za Rais katika kuliongoza taifa letu.
Mhe. Kilango aliongeza kuwa kabla ya Rais Samia kuanza kuongoza taifa, Jimbo la Same Mashariki lilikuwa na kituo kimoja tu cha afya. Hata hivyo, ndani ya kipindi cha miaka minne, Serikali chini ya uongozi wake imefanikiwa kujenga vituo vinne vipya vya afya katika maeneo ya Vunta, Miamba, Vuji na Mtii.
Kwa msingi huo, Mhe. Kilango alitoa shukrani zake za dhati kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali, kuwathamini na kuwaletea wananchi wa Same Mashariki maendeleo ya kweli yanayogusa maisha yao ya kila siku.