Waarabu watua tena Yanga na fuko la fedha

YANGA imeendelea kuneemeka na kiungo wa zamani wa klabu hiyo, Stephane Aziz KI, huku uhamisho wake kutoka Wydad kwenda Al Ittihad ukiipatia mamilioni ya pesa kutokana na mauzo yaliyofanyika.

Aziz KI ambaye aliitumikia Yanga kwa mafanikio makubwa ndani ya misimu mitatu ambayo ni 2022-2023, 2023-2024 na 2024-2025 akishinda mataji matatu ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA, sambamba na kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022-2023, kwa sasa ni mchezaji wa Al Ittihad ya Libya iliyomnunua kutoka Wydad aliyoichezea kwa takribani nusu msimu tangu ajiunge nayo.

Kiungo huyo raia wa Burkina Faso ambaye alikuwa na kikosi cha Wydad katika michuano ya Kombe la Dunia la Klabu 2025 nchini Marekani, wakati anaondoka Yanga, klabu hiyo iliweka kipengele cha kwamba akiuzwa kuna fedha zinatakiwa ziingie kwenye akaunti yao.

Kwa mujibu wa mkataba huyo wa mauziano kati ya Yanga na Wydad, endapo Aziz KI atauzwa basi Wanajangwani hao wanapata asilimia 20 za mauzo hayo na ndicho kiasi ilichovuna kutokana na kuuzwa kwa dau la Dola 500,000 (Sh1.3 bilioni).

“Yanga imepata Dola 100,000 (tariban Sh254.4 milioni) kutoka Wydad ambapo imemuuza Aziz KI kwenda Libya kwa kiasi cha Dola 500,000 (Sh1.3 bilioni). Hii ni kutokana na makubaliano ya kimkataba ambayo wamewekeana,” kimedai chanzo kutoka Yanga.

Chanzo hicho kimeongeza kwamba, makubaliano hayo yalikuja kufuatia Aziz KI wakati anauzwa, alikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na Yanga, hivyo ndani ya muda huo, endapo timu nyingine ikihitaji kumnunua, ndipo Yanga inapata asilimia 20. Baada ya hapo, hakuna fedha nyingine itakayoingiza. Ikumbukwe kuwa, Aziz KI akiwa Yanga aliyojiunga nayo Julai 2022 akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast, alifunga mabao 39 katika Ligi Kuu Bara ndani ya misimu mitatu. Ule wa kwanza alifunga tisa, wa pili 21 akiibuka kinara wa mabao na wa tatu alitoka nayo tisa.

Aziz KI anaiacha Wydad ikiwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipangwa kundi B sambamba na Azam FC, AS Maniema na Nairobi United, ambapo tayari amecheza mechi mbili kati ya tatu hatua ya makundi.

Al Ittihad ndiyo timu inayoshika nafasi ya kwanza kwenye kundi la pili la Ligi Kuu Libya kwa sasa, ikiwa imecheza mechi tano na kukusanya pointi 15.

Aziz KI anaungana na Thembinkosi Lorch raia wa Afrika Kusini ambaye naye ametua hapo akitokea Wydad katika kipindi hiki cha usajili wa Januari 2026.