UMEIKATIA tamaa Simba katika harakati za kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu? Kama ni hivyo, basi msikie kocha mkuu Steve Barker alichosema kuelekea mechi ya Jumapili hii dhidi ya Esperance na zile zingine zilizobaki katika kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika.
Barker baada ya kuiongoza Simba katika mechi moja ya makundi na kupoteza ugenini kwa bao 1-0 dhidi ya Esperance iliyofanya timu hiyo sasa kufungwa zote tatu, alisema kikosi chake kitaendelea kupigana huku akija na mpango mwingine wa kukabiliana na Waarabu hao.
Simba imepoteza mechi tatu za kwanza za Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, ikiwa ni rekodi mbovu zaidi kwa Wekundu hao tangu ilipoanza kushiriki makundi ya michuano ya CAF 2003, hali inayohatarisha nafasi yao ya kutinga hatua ya robo fainali.
Hata hivyo, hatua ya mwisho kwa Simba kujipima juu ya matokeo hayo itakuwa Februari Mosi, 2026 itakaporudiana na Esperance de Tunis kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, lakini kabla ya hapo, leo Alhamisi itacheza mechi ya Ligi Kuu Bara itakapokuwa mwenyeji wa Mashujaa ya Kigoma.
Akizungumza na Mwanaspoti, Barker alisema hawana sababu ya kukata tamaa kwa kuwa wana nafasi ya kufanya vizuri, ambapo itakapokuwa nyumbani itakuja na nguvu ya kutafuta ushindi wa kwanza kwenye mechi hizo za makundi.
Alisema wanafahamu makosa yaliyotokea kwenye mchezo wa ugenini na kwamba wataitumia mechi ya ligi kutafuta mabadiliko, kisha kuanza kujiandaa kupambana na Waarabu hao.
“Kukata tamaa? Hapana, hatuwezi kufanya makosa hayo. Tuna nafasi, ingawa ukiangalia sisi na timu zilizo juu kuna utofauti. Tunahitaji kubadilisha mambo, hii si timu ambayo tunatakiwa kuendelea kuona inapoteza matokeo mazuri.
“Tuna wachezaji ambao wanaimarika kwa haraka. Ukiangalia mechi iliyopita tulikuwa na kitu bora hadi katikati ya uwanja, lakini kuna eneo la robo ya mwisho tulishindwa kuwa na nguvu kubwa ya kufanya kitu kikubwa zaidi,” alisema.
Barker aliongeza kuwa, anavutiwa na namna wachezaji wake wanavyoonyesha uwezo wa kufanya mambo makubwa, huku wale wapya wakiongeza kitu kwenye kikosi hicho, ambapo anaamini baada ya muda wanaweza kuwa na kikosi bora.
“Tuna wachezaji wengi wapya, lakini ndani ya siku chache kuna kitu tofauti wamekiongeza kwenye timu. Baada ya muda tunaweza kuwa na timu nzuri ambayo itafanya vizuri zaidi,” alisema Barker.
“Tuna mchezo wa ligi, tutautumia kurekebisha baadhi ya mambo kwenye kikosi. Tutakuwa na sura tofauti ya ubora tutakapokutana na Esperance. Tunahitaji kushinda hiyo mechi, bahati nzuri tutakuwa mbele ya mashabiki wetu.”
Hakuna kingine ambacho Wanasimba wanakihitaji kwa sasa zaidi ya kuiona timu yao ikipata ushindi kwani imekosa fursa hiyo katika mechi tatu mfululizo.
Mara ya mwisho Simba kupata ushindi ilikuwa Januari 5, 2026 ilipoichapa Fufuni mabao 2-1 katika hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi 2026.
Baada ya hapo, imefungwa 1-0 na Azam katika nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026, kisha sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu Bara na kichapo cha 1-0 katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance ikiwa ni mechi ya kundi D.
Leo Alhamisi, ni nafasi ya Simba kurudisha hali ya ushindi ndani ya kikosi wakati timu hiyo ikikabiliana na Mashujaa katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mashujaa nayo si kinyonge, kwani inahitaji kufanya vizuri kurekebisha pale ilipokosea katika mechi tatu zilizopita kwani haijapata ushindi wala kufunga bao, ikiambulia suluhu mbili dhidi ya Coastal Union na Dodoma Jiji, kisha ikapoteza kwa kipigo kizito cha mabao 6-0 dhidi ya Yanga.
Mashujaa kabla ya hapo, ilishinda mechi mbili mfululizo dhidi ya Mbeya City (1-0) na Namungo (1-0), hivyo mechi ya leo kwao na Simba, ina kitu cha kukiangalia zaidi.
Rekodi zinaonyesha kuwa, katika Ligi Kuu Bara, timu hizo tayari zimekutana mara nne huku Simba ikiibuka na ushindi zote, ikifunga mabao sita na Mashujaa ikipata bao moja.
Ukiangalia msimamo wa Ligi Kuu Bara, timu hizi zimelingana pointi zote zikiwa na 13, lakini Simba imecheza mechi sita ikiwa nafasi ya sita, huku Mashujaa ikiwa nazo kumi ikikamata nafasi ya nane.
Kocha wa Mashujaa, Salum Mayanga alisema baada ya kutoka kufungwa mabao 6-0 na Yanga, hali ilikuwa mbaya ndani ya kikosi kutokana na saikolojia ya wachezaji kuvurugika, lakini ameweka mambo sawa.