Dodoma. Sakata la ufisadi kwa vigogo wakiwamo mawaziri limeibuliwa bungeni na mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby akisema Tanzania bado ina mafisadi wengi na wanakula kuliko inavyodhaniwa.
Mbunge huyo amekwenda mbali zaidi akisema yuko tayari kuwataja kwa majina yao kama itahitajika huku akiwataka wasaidizi wa Rais Samia Suluhu Hassan kumsaidia ipasavyo na kuachana na mipango ya kujipanga na urais mwaka 2030.
Suala la ufisadi ambalo ameliibua Shabiby bungeni leo Jumatano, Januari 28, 2026 wakati akichangia hotuba ya Rais Samia aliyoitoa alipolizindua Bunge la 13, Novemba 14, 2025, si jipya kwa kuwa, limekuwa likizungumzwa mara kadhaa na viongozi wakuu.
Si viongozi wakuu tu akiwamo Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba na kutangaza kuwashughulikia ambao watakuwa wanabainika, hata ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) za kila mwaka zimekuwa zikiibua ufisadi serikalini.
“Mimi kwenye ukweli huwa nazungumza ukweli na kwenye kona huko huwa siendi,” amesema Shabiby akianza kuchangia hotuba hiyo huku akipongeza miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni mwake ikiwamo ya afya na elimu.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia moja ya mambo aliyosisitiza ni kuunda Serikali itakayokuwa na uwajibikaji na mwenendo wa kuwatumikia wananchi ili mwisho wake watu wapate tabasamu.
Shabiby ambaye amekuwa mbunge wa Gairo tangu mwaka 2005 amesema: “Katika nchi hii, sasa hivi mafisaidi wanapiga, siyo wanapiga kidogo, wanapiga kwa uhakika, ni walaji na ni walafi.”
Amesema watu hao wanafanya mambo hayo wakidhani wananchi hawana uelewa, akitolea mfano vijiwe vya bodaboda ukienda unakutana na wenye elimu ya kidato cha nne, sita, chuo kikuu, darasa la saba na wasiosoma na wanapokaa pamoja na kuzungumza wote wanakuwa chuo kikuu.
“Sasa utakuta mtu yuko serikalini ana GPA 2.5 halafu yule bodaboda ana GPA 4, halafu huyu jambazi anamtuma bodaboda mwenye GPA ya 4 kwamba peleka misumari pale, pelaka hapa, hafu huyu bodaboda mjanja anajua mshahara wake,” amesema Shabiby.
Hata hivyo, Katibu wa waendesha bodaboda kituo namba 6 Kisasa, Ayub Leon amekiri kwenye shughuli hiyo wapo wasomi na kweli wanajua kinachoendelea katika baadhi ya maeneo mengi.
“Mheshimiwa Shabiby amezungumza kweli, mimi hapa nina Stashahada (Diploma) ya Utawala kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa, lakini kwenye kijiwe chetu wapo watu wanashahada mmoja mwalimu na mwingine ofisa mipango, kwa hiyo tunatambua mengi,” amesema Leon.
Dereva huyo ameitaka Serikali kutazama vipato vya watu na kufuatilia maendeleo yao ndipo watabaini kuna ufisadi mwingi na matumizi ya anasa huko mitaani kwa kuwa, kuna watu wanafunga mitaa.
Akiendelea kuzungumza bungeni, Shabiby amesema kama sheria za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) hazina meno zipelekwe bungeni ili zibadilishwe huku akitoa wito kwa wabunge wa CCM kuzungumza ukweli si ya leo pekee bali hadi ya mwaka 2030.
Mbunge huyo amesema urais ni taasisi akimaanisha hata Rais Samia apambane vipi kama wasaidizi wake hawamsaidii vizuri hakuna kinachoweza kufanyika.
“Hivi hawa wa chini wanaona haya yanayofanyika? Mimi ni mfanyabiashara sipendi ufisadi na sipendi wezi, kwa sababu mimi miaka mingi nafanya biashara, nanunua hiki, nanunua kile, kinakuja kitu kinaiba kinaingia kwenye biashara zako.
“Unangoja kifirikishe, kitafirisika tu lakini miaka mitano, sita imekwisha kukuumiza. Mheshimiwa Waziri Mkuu (Dk Mwigulu) tunaona unahangaika na umeanza vizuri sana kwenye masuala haya, basi endelea,” amesema.
Katika kusisitiza hilo, Shabiby huku akisikilizwa kwa umakini na wabunge wenzake akiwamo Dk Mwigulu akasema: “Kuna mafisadi wengi tena wakubwa, watu wanajenga nyumba kila kukicha na wengine wanasubutu hata kuandika majina kwenye nyumba zao, hivi hili hamlioni ama mnataka nani aseme, watu wanaona.”
Mbunge huyo ameeleza namna upigaji unavyofanyika hadharani huku akihoji hatua gani zinachukuliwa huku akimpongeza Dk Mwigulu kukutana na watu wa Sekretarieti ya Maadili ya Utumishi wa Umma.
“Watu wa maadili wako wapi, wanakuja kutufuata sisi wabunge ambao hatuna fedha za Serikali, mbunge mimi nakutana na fedha ya Serikali wapi popote? Lakini ninyi mawaziri na watu wa chini ndiyo mnakutana na fedha kwa hiyo kama ni vibaka ni huko kwenye chini,” amesema Shabiby.
Amesema Rais hawezi kuangalia wezi Gairo, Bukombe au kwingineko na kuwaomba wasaidizi hao wa Rais kuwa wanafuata ushauri wa kitaalamu kama vyombo vya ulinzi ambavyo vinahusika kwenye ushauri na muuzingatie.
“Kwa sababu wananchi wa sasa hivi, wanajua kabisa hili jengo la fulani, hiki kitu cha fulani, yuko serikalini, ni mwizi aliyekubuhu na wengine wanakwenda hawana aibu, wanawanunulia mishikaki, wanawanunulia nini,” amesema.
Katika kusisitiza hilo, Shabiby amesema: “Kama hamna njooni nitawaandikia, msiwe na wasiwasi, lakini katika kitu kinazungumzwa na mama alikizungumza hapa na alikizungumza kwa uchungu sana, anataka usaidizi kutoka kwa wasaidizi wake.”
“Na huko mawaziri, msikae tu mnangoja nani atakuwa Rais baada ya mwaka 2030, hata sisi huku nyuma tulikuwa tunaongea…na hata mimi natosha, yupo mwingine anataka uwaziri mkuu 2030,” amesema Shabiby.
Kingine amesema ndani ya Bunge wapo watu wanashindwa kusema ukweli na hivyo hawamsaidii Rais bali yeye ameamua kuwa mkweli na mtu ambaye hatasema kinafiki katika jambo ambalo analiamini.
Novemba 13, 2026, Dk Mwigulu alitangaza anakuja na fyekeo na rato kwa watumishi wazembe na wala rushwa na lazima washughulikiwe.
Dk Mwigulu alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya jina kupelekwa bungeni na mpambe wa Rais (ADC), Brigedia Jenerali Nyanburi Nashauri na kupigiwa kura 369 kati ya 371 za ndio.
“Nawapa salamu watumishi wazembe na wala rushwa, nakuja na fyekeo na rato, Serikali haitavumilia uzembe, rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, hao watu wakae mguu sawa,” alisema Dk Mwigulu.
Waziri Mkuu alirudia kauli tena alipozungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Maadili Desemba 11, 2025 alipoagiza viongozi wa umma kuorodhesha mali zao.
“Sensa ya kuorodhesha mali inakuja, lazima tukubali kuwa nchi hii inahitaji watu wenye kuitumikia kwa dhati na haki, tena nilitaka kutangaza kazi hiyo kuanza mara moja lakini nikasema ngoja nisubiri kwanza,” alisema Dk Mwigulu.
Katika michango yao kwenye hotuba hiyo, baadhi ya wabunge wanataka Serikali ishughulike na mafisadi zaidi ikiwemo kutumia kauli mbiu ya Waziri Mkuu aliposema atakuja na fyekeo.
“Mheshimiwa waziri mkuu, nilikusikia katika hotuba yako mwanzo ukisema utakuja na fyekeo, na mimi naomba lifanye kazi kwa wazembe wasioitakia mema nchi yetu, na iwe sasa hapana kusubiri,” amesema mbunge wa Ushetu (CCM), Emmanuel Cherehani.
Mbunge huyo amesema kama itabidi, fyekeo likaanzie kwa watumishi watakaokwamisha mpango wa bima ya afya kwa wote, kwa kuwa ana shaka huko kutakuwa na mkwamo.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (ACT-Wazalendo), Kiza Mayeye amewataka viongozi waliopewa dhamana kuwajibika kwa wananchi na wapambane kwa kutazama masilahi mapana ya Taifa kuliko kujinufaisha wenyewe.
Mayeye amesema ndani ya chama chao walikuwa na sera ya uwajibikaji kwa viongozi na wananchi kila mtu na kipande chake, hivyo hakuna namna bora viongozi wasimame katika nafasi zao ili kutimiza wajibu.
Wakati Shabiby akitoa kauli hiyo, Mbunge wa Mvomero (CCM), Sarah Msafiri amesema kumekuwa na ubabaishaji mkubwa wa ukosefu wa maji vijijini kunakosababisha migogoro ya Wafugaji na wakulima.
Naye Spika wa Bunge, Mussa Zungu ameitaka Serikali kutazama mifumo yake hasa kwa Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa, watu wanalipishwa gharama kubwa wakati hawatumii maji.
“Serikali angalieni katika Jiji la Dar es Salaam watu hawatumii maji, kila wakati yamekatika lakini wananchi wanapelekewa bill (ankara) kubwa ambazo zinatia shaka,” amesema Zungu.
Akijibu kauli ya kukosekana kwa maji baadhi ya maeneo hasa vijijini, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema Serikali imetenga Sh1.8 bilioni kwa ajili ya kufanya maboresho katika miradi ya majini maeneo ya vijijini.
Aweso amesema jumla ya vijiji 1,575 vimefikiwa na huduma hiyo kupitia miradi 878 wakati kwa upande wa mijini iko zaidi ya miradi 200 inayoendelea kutekelezwa.
Hata hivyo, ametaja mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa kichocheo na chanzo cha upungufu wa maji, akaeleza kwamba Serikali haioni gharama katika utekelezaji wa miradi hiyo badala yake inachojali ni wananchi kupata maji.