Sababu Gen Z kuzeeka haraka kimwonekano kuliko Milenia

Dar es Salaam. Licha ya kuwa kizazi changa zaidi, tafiti na uchunguzi wa wanasayansi na wataalamu zinaonesha k vijana wa kizazi cha Gen Z wanaonekana kuzeeka haraka zaidi kimwili, kisaikolojia na hata kijamii kuliko kizazi cha Milenia.

Kizazi cha Gen Z, ni wale waliozaliwa kuanzia mwaka 1997 hadi 2012, huku kizazi cha Milenia kikiwa ni wale waliozaliwa kati ya miaka ya 1981 hadi 1996.

Hali hiyo imezua mjadala mpana duniani, huku wataalamu wakibainisha kuwa sababu zake hazihusiani moja kwa moja na umri wa kibaiolojia, bali mazingira, mtindo wa maisha na mzigo mkubwa wa changamoto wanazokutana nazo tangu wakiwa wadogo.

Tafiti kadhaa za kimataifa zinaonesha Gen Z ni miongoni mwa vizazi vinavyokumbwa zaidi na msongo wa mawazo, wasiwasi na sonona wakiwa katika umri mdogo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) na taasisi za utafiti wa afya ya akili zinaeleza kuwa msongo wa mawazo wa muda mrefu huongeza homoni ya cortisol mwilini, ambayo imehusishwa na kuharakisha kuzeeka kwa seli za mwili.

Msongo huo umetajwa kuchangiwa na mambo kadhaa, ikiwamo hofu ya mabadiliko ya tabianchi, ugumu wa maisha na ajira, shinikizo la mafanikio ya haraka na mabadiliko ya kasi ya kijamii na kiteknolojia.

Kwa mujibu wa wataalamu, Milenia walipitia changamoto hizi wakiwa watu wazima zaidi, tofauti na Gen Z ambao wamezikuta tangu utotoni.

Gen Z ndicho kizazi cha kwanza kukua kikizungukwa na simu janja, mitandao ya kijamii na teknolojia ya intaneti tangu wakiwa watoto.

Makala ya kitaalamu iliyochapishwa kwenye tovuti ya MDLinx Agosti 12, 2024 ilionesha kuwa matumizi makubwa ya skrini yanahusishwa na kukosa usingizi wa kutosha, uchovu wa macho na mwili, kukaa muda mrefu bila mazoezi na kuchoka kiakili mapema.

Ukosefu wa usingizi, kwa mujibu wa wataalamu wa afya, ni miongoni mwa sababu kuu zinazoharakisha dalili za kuzeeka, ikiwamo ngozi kuchoka, mwili kudhoofika na kupungua kwa kinga.

Shinikizo la mitandao ya kijamii

Tofauti na Milenia, Gen Z wamekua wakikumbana mapema na maudhui yanayohusu kuzeeka, urembo na taratibu za vipodozi kama Botox na fillers, ambavyo sasa vimeanza kuonekana kama jambo la kawaida hata kwa vijana wa chini ya miaka 25.

Mitandao ya kijamii pia imeongeza hali ya kujilinganisha na wengine, huku picha zilizochujwa (filters) na kamera zenye ubora wa juu zikifanya mabadiliko madogo ya mwili yaonekane makubwa zaidi.

Wataalamu wanasema hali hiyp inasababisha vijana kujiona wanazeeka mapema, hata kabla dalili halisi hazijajitokeza.

Tafiti pia zinaonesha kuwa ulaji zaidi wa vyakula vilivyosindikwa, kula kwa mpangilio usioeleweka na kupungua kwa shughuli za nje kama michezo, vimetajwa kuchangia kuonekana kwa uchovu wa mapema.

Uchunguzi unaonesha kuwa vijana wengi wa Gen Z wanaripoti kuhisi uchovu wa maisha mapema, hali ambayo awali ilionekana zaidi kwa watu wazima waliokuwa kazini kwa miaka mingi.

Wataalamu wanaeleza kuwa kupungua kwa michezo ya asili utotoni, muda mwingi wa kukaa ndani na utegemezi mkubwa wa teknolojia, kumeathiri uimara wa kimwili na kiakili wa kizazi hiki.

Tafiti zinaonesha ongezeko la matumizi ya sigara za kielektroniki miongoni mwa Gen Z. Nikotini, huchangia kuharibu mzunguko wa damu, kuzeesha ngozi mapema na kudhoofisha afya kwa ujumla.

Rais wa Chama cha Madaktari Bingwa wa Moyo Tanzania (TCS), Robert Mvungi, anataja mambo yanayosababisha maradhi ya moyo kuwa ni unene kupita kiasi, matumizi ya pombe kupita kiasi, sigara, shisha, msongo wa mawazo na ugumu wa maisha, huku pia shinikizo la damu likichangia.

“Tunapokea vijana wadogo sasa hivi, wenye umri wa miaka 20 hadi 40, wenye magonjwa ya moyo na wengine hadi figo zimefeli. Haya ni magonjwa ya wazee, si vijana.

“Wengi wamekuwa na matumizi mabaya ya pombe, sigara na shisha. Shisha kama kuna tumbaku imewekwa mule ndani inaathiri zaidi lakini kitu chochote unachokilazimisha kwenda kwenye mapafu kikiyaathiri kwa kiasi kikubwa moyo nao unaathirika,” anasema.

Ephrahim (30) anasema kilichochangia Gen Z kuwa na mwonekano wa kuzeeka haraka ikilinganishwa na Milenia ni ugumu wa maisha.

“Maisha yetu hatujaishi kama zamani. Wengi hawazifikii fursa, watu wanakuwa na matarajio makubwa lakini hawayafikii,” anasema.

Diana Songa ameunga mkono utafiti huo, akisema sababu zilizotajwa zinawiana kwa namna moja ama nyingine, akifafanua kuwa kwa sasa unaweza kukutana na kijana aliyemaliza chuo lakini ana miaka mitano nyumbani.

“Kijana huyu anaamua kwenda kufanya kazi nyingine, anafanya kazi ngumu kwa hela kidogo. Anapambana sana, ana familia, anahitaji fedha. Amepata Sh7,000, familia inahitaji Sh14,000,” asema.

Diana anasema Gen Z hawana utaratibu wa mazoezi, na wanapofikiria kufanya hivyo, shughuli zingine zisizo na tija zinaingilia maisha yao, ikiwamo mitandao, kuangalia filamu, lakini pia ulaji wa vyakula visivyo asili na vilivyopitia mchakato usioshauriwa kitaalamu.

Gen Z wameingia katika utu uzima wakati dunia ikikumbwa na changamoto kubwa, ikiwamo janga la Uviko-19, kupanda kwa gharama za maisha na kuyumba kwa soko la ajira.

Makala ya sayansi iliyochapishwa kupitia jarida la kisayansi la PubMed iligundua kuwa wakati wa mwanzo wa janga la Uviko-19, vizazi vya Gen Z vilipata dalili mbaya zaidi za afya ya akili na msongo wa mawazo ikilinganishwa na vizazi vingine.

Tafiti zinaonesha kuwa shinikizo la kiuchumi lina mchango mkubwa katika kuharakisha kuzeeka kwa mwili kutokana na msongo wa mawazo wa muda mrefu.

Wataalamu wanasisitiza kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja unaothibitisha kuwa Gen Z wanazeeka kibaiolojia haraka kuliko Milenia.

Hata hivyo, mazingira wanayoishi, shinikizo la kijamii, maisha ya kidijitali na changamoto za kiuchumi vinawafanya waonekane na kujihisi kuzeeka mapema.

Kwa ufupi, Gen Z hawazeeki haraka zaidi, bali wanaishi maisha yenye mzigo mkubwa zaidi wakiwa bado vijana.