Tanford kuipigia chapuo Tanzania kongamano la biashara, usafirishaji Dubai

Dara es Salaam. Jukwaa la Kitaaluma la Umoja wa Wamiliki wa Kampuni za Usafirishaji na Mizigo za Watanzania wanaofanya kazi Dubai na soko la kimataifa (Tanford) limeandaa kongamano la siku mbili litakalofanyika Dubai, Umoja wa Nchi za Kiarabu Februari 13 na 14, 2026 kwa lengo la kuinadi Tanzania katika soko la kimataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 28, 2026, Mwenyekiti wa Tanford, Hussein Jamal amesema kongamano hilo lijulikanalo kama Tanzania Trade and Logistics Forum 2026 litaleta pamoja wadau wa biashara na usafirishaji ili kufungua fursa za kibiashara kati ya Tanzania na Dubai.

Amesema kongamano hilo linalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usafirishaji Afrika Mashariki na Kati, sambamba na kukuza matumizi ya bandari na miundombinu ya usafirishaji kwa kukusanya mizigo ya masoko ya kimataifa kupita Tanzania.

Jamal ameongeza kuwa kongamano hilo litasaidia bidhaa za Kitanzania kupata masoko mapya kimataifa, huku Tanford ikisimama kama daraja la kibiashara kati ya Tanzania na soko la dunia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dk Latifa Khamis amewahimiza wafanyabiashara wa Kitanzania kushiriki kongamano hilo akisema litafungua fursa za ushirikiano na wafanyabiashara wa kimataifa.

Naye Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa), Edwin Urio amesema kongamano hilo ni fursa ya kukuza biashara na uchumi wa nchi, akibainisha kuwa sekta ya usafirishaji na logistics ni miongoni mwa zinazoingiza fedha nyingi za kigeni nchini.