Athari za kukaa kimya ukiwa na deni la mtu

Kwa watu wengi katika jamii ya Kitanzania, kukopeshana fedha ni jambo la kawaida katika kutatua changamoto za maisha ya kila siku. Hata hivyo, kumekuwepo na mwenendo usio mzuri ambapo baadhi ya wanaokopa, wanaposhindwa kurejesha fedha kwa muda walioahidi, huamua kukaa kimya bila kutoa taarifa yoyote.

Tabia hii si nzuri, kwani huathiri uaminifu wa kijamii na kudhofisha mahusiano baina ya watu.

Katika jamii yetu, tunakopeshana kwa mambo mbalimbali mfano kama ada, nauli, chakula, au huduma za nyumbani. Mathalan, masokoni utasikia “niazime buku nitoe chenji”, kwa jirani “niazime hela niweke LUKU, asubuhi nitakurudishia”, dukani kwa Mpemba umekopa unga wa ngano, au mwanafunzi “niazime hela nikale, baadaye nikitumiwa nitakurudishia”. Na mengine.

Haya yote ni mifano halisi ya namna kukopeshana kunavyokuwa sehemu ya maisha yetu ya kawaida.

Mara nyingi mikopo hii midogo haina makubaliano ya maandishi wala haina riba, dhamana yake ni urafiki, undugu, ujirani, ukaribu wa kikazi, nk. Hii ndiyo sababu mikopo hii huwa nyenzo muhimu na ya haraka ya kusaidiana kijamii.

Hata hivyo, uzoefu wa maisha unaonesha changamoto moja inayojitokeza mara kwa mara: mtu anakopa, anakubaliana muda wa kurejesha, lakini muda unapofika hashughulikii deni wala kutoa taarifa, bali anakaa kimya kana kwamba hakuna kilichotokea.

Wapo wanaoweza kulipa lakini hawalipi mpaka wakumbushwe, utasikia “aisee, nakulipa nilikuwa nimesahau”, au si ajabu akaomba muda mwingine “basi nitakuletea”. Unaweza kujiuliza nisingemuliza ingekuwaje?. Kiuhalisia, tabia hii ni ishara ya wazi ya kupuuza wajibu wa kifedha. Wapo pia ambao, ikitokea hujakumbusha, hawalipi kabisa.

Katika hali zote mbili, tabia hii si nzuri kuendekezwa, kwa sababu inavunja imani ya kusaidiana na huleta athari kwa mkopaji na mkopeshaji.

Kwanza, kutokutoa taarifa hupunguza kuaminika. Ni kweli mambo yanaweza kwenda tofauti na mipango, lakini ukimya ni sawa na kukwepa uwajibikaji.

Hata ujumbe mfupi tu wa kusema “nimekwama kidogo ndugu yangu” unaonesha heshima na uwajibikaji. Mtu anapozoea kukaa kimya, taratibu hupoteza mtaji wake wa kijamii; siku atakapohitaji msaada tena, anaweza asiuone kwa urahisi.

Pili, kukaa kimya kunaweza kuharibu mahusiano ya kijamii. Katika jamii zetu, kuazimana fedha kunabeba heshima na ukaribu. Mkopaji anapojisahaulisha, humweka aliyemkopesha katika wakati mgumu: je, amkumbushe au akae kimya?.

Ikitokea amemkumbusha kwa bahati mbaya wakapishana maneno, na uhusiano unaanza kuingia doa. Wakati mwingine mkopeshaji hulazimika kubeba hasara kimya kimya ili kulinda urafiki au undugu. “jamaa namuheshimu wacha tu akitaka atanilipa”.

Tatu, tabia ya kukaa kimya hujenga utamaduni hatarishi wa kifedha. Inawafundisha watu mbinu za kukwepa kulipa, mfano mtu anaamua tu kusema “Ijumaa nitakupa hela yako” ilhali anajua wazi hatafanya hivyo. Ijumaa inapofika, anakaa kimya, na maisha yanaendelea kana kwamba hakuna tatizo.

Nne, kwa hofu ya kutorudishiwa, jamii huanza kukosa moyo wa kusaidiana katika dharura. Mtiririko wa msaada wa kijamii unapungua, umoja unadhoofika, na huibuka lawama zisizo sahihi ambazo baadaye zinakuwa chuki na uhasama, “fulani ana uwezo lakini hataki kusaidia wenzake”, ilhali chanzo halisi ni kupotea kwa uaminifu.

Ninachosisitiza ni kuwa kushindwa kurejesha fedha kwa wakati ni jambo linaloweza kumkuta yeyote. Lakini kushindwa kulipa na kisha kukwepa kwa kukaa kimya bila taarifa ni kukiuka maadili ya kijamii na kuharibu msingi wa kusaidiana katika jamii.