Wawili wachomwa moto Songwe wakidaiwa kuiba ng’ombe

Songwe.Watu wawili wameuawa na wananchi wenye hasira katika Kijiji cha Isalalo, wilayani Mbozi, kwa tuhuma za wizi wa ng’ombe wanane wanaodaiwa kuibwa wilayani Momba.

Katika tukio hilo, wananchi wamechoma moto na kuteketeza gari aina ya Fuso lililokuwa limebeba mifugo hiyo, huku ng’ombe hao wakidaiwa kutoroshwa na watu wasiojulikana baada ya vurugu hizo kutokea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, SACP Augustino Senga, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa wanamshikilia dereva wa gari hilo, Kennedy Mwaluvanda mkazi wa Nanenane jijini Mbeya kwa mahojiano zaidi.

Kamanda Senga amesema dereva huyo alikuwa anaendesha gari lililokuwa limebeba ng’aombe hao, mali ya Aseneje Mkumbwa mkazi wa Mbeya.

Aidha Kamanda Senga amesema jeshi hilo litafanya msako mkali kuhakikisha linawatafuta na kuwakamata watu wawili ambao hawajafahamika majina yao wanaodaiwa kuhusika kwenye wizi huo na mpaka sasa hawajulikani walipo.

“Miili imepelekwa hospitali, Jeshi la Polisi limeanzisha msako mkali kuwatafuta watu wengine waliohusika katika wizi huo pamoja na wale waliochukua sheria mkononi, tunatoa wito kwa jamii kuacha vitendo vya kujichukulia sheria mkononi”, amesema Kamanda Senga.

John Ankulikwa mkazi wa kijiji cha Isalalo amesema watu  waliuwawa na wananchi wenye hasira  baada ya kupewa taarifa ya wizi wa ng’ombe kutoka Momba. “Wananchi walipopata taarifa hiyo  walikusanyika kwa ajili ya doria na kufanikisha kuwakamata wawili hao na kuwachoma moto.”