Saa chache baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuufungia Uwanja wa KMC Complex, sababu mbili zimetajwa kusababisha maamuzi hayo, huku ishu ya Kibwana Shomary kubebwa na baunsa ikiwemo.
TFF imeufungia uwanja huo ambao umekuwa ukitumiwa na timu za Yanga na KMC kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu Bara kwa kile ilichoeleza kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.
Taarifa hiyo ilieleza zaidi kuwa miundombinu ya uwanja huo haikidhi matakwa ya kikanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya kanuni ya leseni za klabu nchini.
Hata hivyo, kumekuwa na sintofahamu mitandaoni baada ya mashabiki kudai kuwa Uwanja wa KMC una ubora mkubwa kuliko viwanja vingi vya soka kwa sasa na bado haijafahamika sababu haswa ya kufungiwa kwake.
Baada ya taarifa hiyo, chanzo ndani ya TFF kimetaja sababu mbili za kufungiwa uwanja huo, moja ikiwa kutokana na kukosekana kwa njia muafaka wa gari la wagonjwa na kusababisha mchezaji wa Yanga Kibwana Shomary alipopata tatizo la afya kwenye mchezo uliopita dhidi ya Dodoma kubebwa juujuu hadi kwenye gari nje ya uwanja.
Wakati mchezo huo ulipomalizika kati ya Yanga dhidi ya Dodoma Jiji, Kibwana alipata shida ya afya na kujikuta anabebwa mikononi akipelekwa kwenye gari kisha kuwahishwa hospitali kwa matibabu zaidi.
“Lile tukio la mgonjwa kubebwa kwenye mikononi haikuwa sawa na shida pale ni kwamba ile njia ya kupita gari ipo tofauti sana na kule ambapo vyumba vya kubadilishia nguo vilipo, ndio maana unaona mchezaji akabebwa kwa njia ambayo ni hatari,”alisema bosi huyo.
Sababu ya pili iliyopelekea maamuzi hayo ikatajwa kuwa mifereji ya maji machafu kushindwa kuhimili kiwango cha uzalishwaji wa maji taka na kusababisha chemba kufurika kila wakati pembeni ya uwanja huo.
“Kule nyuma nako kapiteni muone kila wakati zile chemba zinajaa maji, kumbukeni ule uwanja unatumiwa na timu zenye mashabiki wengi, maji kutiririka vile tena yale machafu sio kitu sahihi, tumewaambia warekebishe.”
Aidha kigogo huyo aliongeza kuwa changamoto hizo walishawahi kuwataka wamiliki wa uwanja huo kuzifanyia kazi kwa muda mrefu lakini bado utekelezaji wake umekuwa sio wa haraka hatua ambayo imewalazimisha kuusimamisha.
“Haya siyo mambo mapya wenyewe wanajua, tumeshazungumza nao sana kufanyia kazi, hata zile taa za nje kiusalama hazitoshi kuna giza kidogo kwa mechi za usiku, shida yao wamekuwa wazito kutekeleza.”
Akizungumzia hilo Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Madenyeka licha ya kugoma kueleza sababu hizo alikiri kupokea maamuzi hayo akisema:
”Ni kweli uwanja wetu umesimamishwa na taarifa itakwenda kwa uongozi na utaangalia namna ya kuboresha yale ambayo yametakiwa na wenzetu wa TFF,” alisema Madenyeka.