MAGARI YA HUDUMA YA NMB YAFIKIA 15 YAKICHOCHEA UJUMUISHAJI WA KIFEDHA

Na Mwandishi Wetu.


Benki ya NMB imeongeza idadi ya magari yake ya kutoa huduma za kifedha hadi kufikia 15, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za benki katika maeneo yenye changamoto ya matawi ya kudumu, hususan vijijini na kwenye maeneo ya biashara yasiyo rasmi.


Ongezeko hilo limetokana na uzinduzi wa magari mapya nane ya Bank on Wheels, ambayo ni matawi yanayotembea yaliyobuniwa kuwafikia wananchi moja kwa moja mahali walipo, ikiwemo vijijini, sokoni na kwenye minada ya mifugo.


Mbali na huduma za kawaida za kibenki, magari hayo pia hutoa elimu ya kifedha, hufungua akaunti, kutoa huduma za mikopo, malipo pamoja na ushauri wa kibiashara, hivyo kurahisisha wananchi kuingia na kushiriki kikamilifu katika mfumo rasmi wa kifedha.


Uzinduzi wa magari hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Ajenda 2030, Mpango Mkakati wa Kati wa NMB kwa kipindi cha 2026–2030, unaolenga kupanua ujumuishaji wa kifedha na kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Akisimamia uzinduzi huo, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, aliipongeza Benki ya NMB kwa mchango wake katika ujenzi wa taifa kupitia matumizi ya suluhisho bunifu yanayolenga kuboresha maisha ya Watanzania wengi zaidi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema magari ya Bank on Wheels yamebuniwa mahsusi kutoa huduma rasmi za kifedha kwa jamii zisizo na matawi ya benki, ikiwemo vijiji vya mbali, masoko na maeneo ya biashara kama minada.


“Haya siyo magari tu, bali ni milango ya fursa. Yanawawezesha wakulima, wafanyabiashara wadogo, wafugaji na wajasiriamali kupata huduma za akiba, mikopo, malipo na ushauri wa kibiashara bila kulazimika kusafiri umbali mrefu,” alisema Bi. Zaipuna.


Aliongeza kuwa huduma hiyo inampunguzia mfanyabiashara muda na gharama za kusafiri kufuata huduma za benki, huku mkulima au mfugaji akipata fursa ya kufungua akaunti na kufanya miamala papo hapo siku ya soko au minada.
Kupitia Bank on Wheels, NMB inaendelea kutekeleza mkakati wake wa Village Banking, unaolenga kupeleka huduma za kifedha karibu na wananchi na kuwajumuisha zaidi katika uchumi rasmi kwa kutumia teknolojia na mifumo ya kidijitali.


Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu (wa pili kulia), akikata utepe kuashiria uzinduzi wa magari nane ya Bank on Wheels (Matawi ya Benki Yanayotembea) yatakayotoa huduma za kibenki mitaani, vijijini na kwenye minada, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Benki ya NMB kumfikia kila Mtanzania mahali alipo. Uzinduzi huo ulifanyika jijini Dar es Salaam. Wa tatu kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna; kulia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Benson Mahenya; wa nne kulia ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Prof. Sylvia Temu, na kushoto ni Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori. (Na Mpiga Picha Wetu)

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu (kulia), na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna (wa pili kulia), mara baada ya kuzindua magari nane ya Bank on Wheels yatakayotoa huduma za kibenki mitaani, vijijini na kwenye minada, kama sehemu ya mkakati wa benki hiyo kumfikia kila Mtanzania mahali alipo. Uzinduzi ulifanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori, na wa pili kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa NMB, Prof. Sylvia Temu. (Na Mpiga Picha Wetu)

……………..