Dawasa yaeleza changamoto, utatuzi wa majitaka Kariakoo

Dar es Salaam. Ujenzi wa maghorofa, hasa unaofanyika usiku bila usimamizi wa kitaalamu, pamoja na biashara ya vyakula umechangia kwa kiasi kikubwa changamoto za majitaka maeneo ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Wamiliki wa majengo na baadhi ya wataalamu wa ujenzi hupeleka michoro ya majengo iliyo sahihi, lakini hubadilisha miundombinu ya majitaka na maji ya mvua kwa siri, kinyume na utaratibu.

Kwa upande wake, wafanyabiashara wa chakula (mama lishe) wamekuwa wakimwaga maji machafu yenye mabaki ya vyakula kwenye mitaro ya maji ya mvua, hivyo kusababisha kuziba kwa baadhi ya mifumo.

Januari 14, 2026, Mhandisi wa Jiji la Dar es Salaam, Isack Mtega, aliliambia Mwananchi kuwa mkakati uliopo ni kupita nyumba kwa nyumba kukagua mifumo ya majitaka, na endapo itabainika imeelekezwa sehemu tofauti, mhusika atatakiwa kuondoa na kuelekeza inapotakiwa.

Majibu hayo yalikuwa yakifuatia habari maalumu iliyofanywa na Mwananchi ikiangazia hali ya majitaka maeneo mbalimbali ya Kariakoo, kama Uhuru, Msimbazi, Sikukuu, Mkunguni na Nyamwezi, ambako kumekuwa na majitaka yanayotiririka barabarani, hali inayosababisha harufu kali na mazingira machafu.

Shimo la majibya mvua likiwa limezibwa baada ya nyumba ya jirani na shimo hilo kujiunganishia kiholela kwa kuingiza mfumo wa maji taka katika mtaa wa Congo na Twiga eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam



Haijalishi ni kipindi cha mvua au kiangazi, kero ya majitaka kutoka kwenye chemba za baadhi ya mitaa ya Kariakoo imeendelea kuwatesa wafanyabiashara, mama lishe na maelfu ya watu wanaofika eneo hilo kwa shughuli za kibiashara.

K`utokana na habari hiyo, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa), jana Jumatano, Januari 28, 2026, ilifanya ukaguzi wa mifumo ya majitaka kujionea hali halisi na kubainisha mikakati wanayoifanya kuhakikisha suluhu inapatikana.

Mhandisi wa Uendeshaji na Matengenezo ya Majitaka, Idara ya Usimamizi wa Usafi wa Mazingira Dawasa, Mbaraka Mpala, amesema changamoto nyingi za majitaka zinazoripotiwa katika maeneo ya Kariakoo na kwingineko jijini hazitokani moja kwa moja na mifumo yao, bali zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na wananchi kuunganisha maji ya mvua kwenye mifumo ya majitaka, kinyume cha utaratibu.

Amesema wapo baadhi ya watu wanaoomba huduma ya majitaka, huku tayari wakiwa wameshajiunganisha kwa namna yao, hivyo ni ngumu kugundulika kwa sababu mifumo iko chini ya ardhi.

Amesema mamlaka hiyo imekuwa ikilaumiwa mara kwa mara pale majitaka yanapofurika, hata katika maeneo ambayo hayahudumiwi na mifumo rasmi ya Dawasa.

Maji taka yakiwa yamezagaa barabarani baada ya nyumba ya kuzibwa kwa bomba lililokuwa linapitisha majitaka kuingizwa kwenye mfumo wa maji ya mvua katika mtaa wa Congo na Twiga eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.



“Changamoto kubwa tunayoipata ni kwamba wananchi wakiona maji machafu au maji yanayotiririka mitaani, wanaamini ni Dawasa moja kwa moja. Hakuna taasisi nyingine wanayoiona zaidi yetu, hivyo mzigo wote tunabaki kuubeba,” amesema Mpala.

Mpala amesema wamejikita katika kufanya usafishaji wa njia za majitaka, ukaguzi wa mara kwa mara na kubaini wateja waliounganishwa kinyume cha sheria, hasa Kariakoo na maeneo yenye msongamano mkubwa wa shughuli za kibiashara.

Hatua hizo, kwa mujibu wa mamlaka hiyo, zinalenga kupunguza matukio ya majitaka kufurika na kuhakikisha mifumo ya majitaka inafanya kazi kwa ufanisi, huku ikitoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka husika badala ya kulaumiana pekee.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mtambani A, Kariakoo, Ally Malima, amesema timu ya Dawasa ilifika mtaa wa Twiga na Congo, eneo lenye kutiririsha maji taka, lakini baada ya ukaguzi wa awali tatizo lilihusiana zaidi na mfumo wa maji ya mvua unaosimamiwa na halmashauri.

“Kulikuwa na ujanja kidogo, watu waliingiza maji machafu kwenye mfumo wa maji ya mvua, hali iliyosababisha ionekane kama ni tatizo la majitaka,” amesema Malima.

Hali hiyo ilisababisha mvutano wa maneno kati ya taasisi husika, kila upande ukieleza kuwa mfumo huo hauko chini ya mamlaka yake moja kwa moja.

Malima amesema hatua muhimu ilipatikana juzi baada ya viongozi wa eneo hilo kuingilia kati, akiwemo mtendaji wa kata, diwani pamoja na wawakilishi wa halmashauri na Dawasa, ilibainika kuwa mfumo ni wa halmashauri, na hivyo jukumu la usafi na marekebisho likabaki kwao.

“Baada ya kukaa pamoja, ikagundulika wazi mfumo ni wa halmashauri. Walia kufanya usafi, na walifanya kazi hiyo usiku ili asubuhi wananchi wakute hali imerekebishwa,” amesema.

Hata hivyo, amedai kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakijitambulisha kama wafanyakazi wa Dawasa bila kuwa na mamlaka halali na kuwahadaa wananchi kwa kuahidi huduma zisizo rasmi.


“Kuna watu wanavaa sura ya Dawasa wakidai wanatoa huduma, kumbe si waaminifu. Wananchi wanaweza kudhani kila kinachofanywa ni halali kisheria, wakati sivyo,” amesema.

Ameongeza kuwa kutokana na wananchi wengi kutokuwa na uelewa wa miundombinu na taratibu za serikali, huwa rahisi kudanganywa na kuingia kwenye makosa bila kujua.

Akizungumza na Mwananchi Januari 28, 2026, Mkurugenzi wa Idara ya Majitaka Dawasa, Lydia Ndibalema, amesema kisheria, mtu anayeingiza majitaka au maji kwenye mifumo bila utaratibu anakiuka sheria za usafi wa mazingira na anaweza kuchukuliwa hatua na mamlaka husika, ikiwemo Halmashauri ya Jiji.

“Sheria ipo waz,; ukikuta mtu ametiririsha majitaka ovyo au ameunganisha bila kibali, anaweza kutozwa faini au kuchukuliwa hatua nyingine. Hata Dawasa tukikutwa tumekiuka, tunaadhibiwa,” amesema Ndibalema.

Amesema wanaofuata utaratibu, kuunganishwa kwenye mfumo rasmi wa majitaka si gharama kubwa, kwani kinachotakiwa ni kuomba kibali, kulipia kiasi kilichopangwa na kuunganishwa kitaalamu.

Hata hivyo, amesema kuna umuhimu wa elimu kwa wananchi, hasa wale wasioelewa taratibu za uunganishaji wa majitaka na matumizi sahihi ya mifumo hiyo.

“Kwa mwananchi asiyeelewa, anafundishwa ili asiingize majitaka au taka ngumu kwenye mifumo; kufanya hivyo ni kujiletea shida mwenyewe na jamii nzima,” amesema.