Dodoma. Serikali imetoa rai kwa wafanyabiashara kutotumia kigezo cha uwepo wa mfungo wa kwaresma na ramadhani kupandisha bei za vyakula kwakuwa ndani ya nchi kipo chakula cha kutosha.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ametoa onyo kwa wafanyabiashara kuwa siyo jambo jema na haipendezi kuona wafanyabiashara wakitumia nafasi hiyo kupandisha bei za vyakula eti kwa kisingizio cha uhaba wa chakula wakati haiko hivyo. Mfungo wa Kwaresma na Ramadhani unatarajiwa kuanza mwezi ujao.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo Alhamisi, januari 29, 20226 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Nancy Nyalusi aliyetaka kujua Serikali imejipangaje kudhibiti mfumko wa bei kupitia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kuelekea mfungo wa Kwaresma na Ramadhani.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ilishatangaza katika msimu wa 2025/26 maeneo mengi ya nchi kutakuwa na upungufu wa mvua jambo lililoilazimu Serikali kutangaza utunzaji wa chakula kwa wananchi.
Hata hivyo, Dk Mwigulu amesema kipo chakula cha kutosha hivyo kuwasihi wafanyabiashara wasitumie kipindi hicho kupata faida iliyopitiliza kiwango ambayo inaweza kuumiza watanzania kwa kisingizio cha tahadhari iliyotolewa na TMA.
“Kwa sasa hatuna upungufu wa chakula, tuna ziada na pale penye tatizo tumeendelea kutatua changamoto hiyo, niwaelekeze wakulima kutunza chakula na wakuu wa mikoa wasimamie kuwakumbusha wakulima wetu kulima mazao yanayostahili ukame na yenye kuhitaji mvua kidogo,” amesema Dk Mwigulu.
Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, mahitaji ya chakula nchini ni tani 150,000 lakini kilichopo kwenye akiba ni tani 400,000 hivyo kuwepo na ziada ingawa akasisitiza kiziuzwe kiholela.