TADB yatenga Sh160 bilioni kupunguza upotevu wa mazao

Dar es Salaam. Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) imetenga Sh160 bilioni kuthibiti upotevu wa mazao baada ya kuvunwa, ikipanga kujenga maghala ya mpunga na mahindi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, wakulima wa Tanzania wanapoteza hadi asilimia 45 ya mazao yao kabla hayajafika kwa mtumiaji wa mwisho.

Licha ya sekta ya kilimo kuajiri zaidi ya asilimia 50 ya wananchi, ripoti nyingine ya Repoa ya Post-harvest losses for marketable fruits and vegetablesya mwaka 2024 ilionyesha wakulima wa mahindi wanapoteza hadi asilimia 47 ya mazao.

Mwaka 2024, sekta hii ilichangia asilimia 18.4 ya pato la Taifa kwa mujibu wa Ripoti ya Mwaka ya Benki ya Tanzania (BoT) ya 2024/2025 na pia iliongoza kwa asilimia 37.6 kama sekta inayovutia zaidi kwa ukopeshwaji.

Akizungumza leo Alhamisi, Januari 29, 2026, Mkurugenzi wa Biashara wa TADB, Afia Sigge na wanahabari kuhusu mwenendo wa utendaji kazi wa benki hiyo, ikiwemo taarifa ya fedha katika kipindi cha mwaka 2025 na mipango ya mwaka huu, alisema:

“Ni eneo tunaloliangalia kwa ukaribu na tunafanya kwa ushirikiano na wadau wengine wanaotuambia ni maeneo gani wakulima wanauhitaji maghala ili tuwajengee,” amesema.

“Pia tumetenga fedha Sh21 bilioni kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora kwenye kilimo cha awali ili kilimo chao kiwe na tija zaidi,” amesema Sigge.

Kwa mujibu wa TADB, tayari wamewezesha ujenzi wa maghala 44 ili kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa.

Mbali na hilo, Sigge amesema zaidi ya wakulima 200,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini wamenufaika na mikopo ya kilimo katika kipindi cha mwaka jana.

Naye Mkurugenzi wa Fedha wa TADB, Kaanaeli Nnko amesema katika kipindi cha mwaka 2025 hadi Desemba 31, benki hiyo imepiga hatua ikiwemo ukuaji wake na kuongeza faida na kutekeleza kwa ufanisi dhamira ya taasisi hiyo.

“Mikopo na dhamana kwa wateja iliongezeka kwa asilimia 51 na kufikia Sh0.81 trilioni, ikionesha mahitaji makubwa ya fedha za maendeleo ya muda mrefu.”

“Ukuaji huu uliwezeshwa na mafanikio katika ukusanyaji wa fedha kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi na kuimarika kwa faida na ufanisi wa uendeshaji,” amesema Dk Nnko.