Tuwaelewe Simba wameamua kuanza upya

SIMBA imeshusha nyota takribani saba wa kigeni katika dirisha hili dogo la usajili huku ikifungulia milango wengine kwa kuwaondoa katika kikosi chake na baadhi bado ipo nao lakini haitowatumia hadi msimu utakapomalizika.

Ni nadra sana kwa timu kufanya usajili wa idadi kubwa hivyo ya wachezaji katika dirisha dogo, lakini Simba yenyewe imeamua kutoangalia historia ikoje na ikaamua kufanya hivyo.

Japo haijatangaza kwamba inaanza upya, hapa kijiweni tunaamini kiuhalisia Simba wameamua kuanza moja jambo ambalo sio dhambi hasa kama timu inaona mambo hayaendi kama ilivyopangwa.

Kimsingi wachezaji ambao wamefunguliwa mlango, hawakuonyesha kwa ukubwa sababu za kuilazimisha Simba kutofanya usajili wa wachezaji wengi wa kigeni dirisha hili dogo la usajili ambalo leo linafikia tamati.

Wengi hawakuwa na viwango tishio ambavyo vingeipa uhakika timu kupata ushindi katika zile mechi ambazo uwezo binafsi wa wachezaji unatakiwa uziamue iwapo mipango na mbinu za benchi la ufundi zinashindwa kufanya kazi.

Na kubwa zaidi Simba haijafanya vizuri katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikipoteza mechi zote tatu za mwanzo jambo ambalo limeiweka katika uwezekano finyu wa kuingia katika hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.

Katika Ligi Kuu tayari wameshaangusha pointi nne huku washindani wao wakubwa Yanga wakiwa wamedondosha pointi mbili tu jambo ambalo linaweka rehani uwezekano wao wa kutwaa taji la ligi hiyo msimu huu.

Ni kama Simba haina cha kupoteza hivyo inaona bora ianze kujenga timu mpya hivi sasa kuliko kusubiri hadi mwishoni mwa msimu ambapo hawa wachezaji iliowanasa pengine wanaweza wasipatikane.