Sabri Kondo, Shillah wawe daraja huko Sweden

AGOSTI mwaka jana, kinda wa Kitanzania, Sabri Kondo alijiunga na BK Hacken inayoshiriki Ligi Kuu ya Sweden akitokea Singida Black Stars na alisaini mkataba wa miaka minne na nusu kuitumikia timu hiyo.

Miezi mitano baadaye, kijana mwingine mdigo wa Kitanzania, Mohammed Shillah naye ametua Sweden katika timu ya AIK ambayo nayo inashiriki Ligi Kuu nchini humo ambapo yeye amesajiliwa kwa mkataba wa miaka mitano.

Klabu zote mbili ambazo wadogo zetu hao wamejiunga nazo ni kubwa pale Sweden na zote zina historia ya kutwaa mataji makubwa nchini humo na kutoa nyota kadhaa waliowahi kutamba katika soka la Ulaya.

Hacken ambayo anachezea Kondo, imewahi kutwaa Ligi Kuu ya Sweden mara moja baadhi ya nyota waliowahi kuichezea timu hiyo ni Benie Traore, Abdoulaye Faye, Kim Kallstrom na Alhassan Kamara.

AIK iliyomchukua Shillah, imewahi kutwaa taji la Ligi Kuu ya Sweden mara 12 na mfano wa nyota maarufu waliowahi kupita hapo ni Magnus Edman, Andreas Andersson, Derek Boateng, Sebastian Eguren, Dickson Etuhu na Olof Mellberg.

Tunaamini kwamba wachezaji wetu Sabri Kondo na Mohamed Shillah wameenda Sweden katika muda na umri sahihi na hapo sio mwisho wa safari yao kisoka bali ni kama njia kwao ya kufika katika Ligi kubwa zaidi Ulaya.

Pia wakati wakitakiwa kupambana ili waonyeshe viwango bora ambavyo vitawafanya wapate malisho ya kijani zaidi, wanapaswa pia kuwa chachu ya mafanikio kwa wenzao.

Kufanya kwao vizuri huko kutafungua fursa ya vijana wa Kitanzania nchini Sweden na hivyo itaiongezea nchi yetu idadi ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi jambo litakalozisaidia timu zetu za taifa.