Serikali yazindua programu ya kupunguza vifo vya mama na mtoto

Dodoma. Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya imezindua programu maalumu kwa ajili ya utekelezaji wa programu hiyo ili kutekeleza mpango wa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wenye umri chini ya miaka mitano,

Programu hiyo ya miaka mitano hadi ifikapo mwaka 2030, itatekelezwa kwenye mikoa ya Geita, Katavi na Kigoma ikiwa na thamani ya dola za Marekani 12 milioni.

Pia, programu hiyo inatajwa kusaidia kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua hadi kufikia vifo 75 kwa vizazi hai 100,000 na watoto wachanga kufikia 12 kwa vizazi hai 1,000 na watoto chini ya miaka mitano kufikia vifo 25 kwa vizazi hai 1,000.

Akizindua programu hiyo leo Alhamisi Januari 29, 2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma za Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk Ahmed Makuani amesema lengo la programu hiyo ni kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwani hata mama mmoja akifariki wakati wa kujifungua, kwao hiyo siyo takwimu bali ni huzuni.

Dk Makuani amesema mpaka sasa Serikali imefanya jitihada mbalimbali za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwani takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kuwa jumla ya akina mama wajawazito 556 kati ya vizazi hai 100,000 walipoteza maisha na hadi kufikia mwaka 2022, idadi ilipungua hadi kufikia vifo 104 kati ya vizazi hai 100,000 sawa na asilimia 80.

“Mkakati wa sasa wa Serikali ni kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, vifo vya watoto wachanga, vifo vya watoto chini ya miaka mitano na suala zima la lishe ni lazima lizingatiwe kwa kuhakikisha kuwa walengwa wanapata lishe bora na siyo zile namba ambazo huwa tunaziona,” amesema Dk Makuani.

Wataalam wa afya waliohudhuria uzinduzi wa program ya kupunguza vifo vya akinamama na watoto wakati wa kujifungua Jijini Dodoma. Programu hiyo inaendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la Thamini Uhai.



Amesema mpaka sasa Serikali imefanya jitihada za kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kutumia mashine za kuwawezesha watoto kupumua (HBB) lakini baada ya hapo watoto hao hawawezi kuendelea kuishi kwani hakuna wataalamu wa kuwafuatilia wakiruhusiwa kwenda nyumbani ambapo wengi wao huwa wanafariki.

“Jitihada za kuwasaidia watoto kupumua baada ya kuzaliwa zimesaidia kupunguza vifo vyao, lakini tukiwaruhusu kwenda majumbani, wale watoto huwa wanafariki kwa homa, kuharisha na nimonia kwa sababu kule hawana wataalamu wa kuwasaidia.

“Hivyo, jitihada ziwekwe kwenye wodi za watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ili kupunguza wimbi la vifo vya watoto hao,” amesema Dk Makuani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika Lisilo la Kiserikali la Tamini Uhai, Banzi Msumi amesema jumla ya dola 12 milioni zimewekezwa katika kusaidia kupunguza vifo vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2030 kwenye mikoa ya Geita, Katavi na Kigoma.

Amesema mradi huo utasaidia kuboresha miundombinu ya afya, kutoa ujuzi kwa wauguzi na wakunga na mafunzo ya watumishi wa afya katika kuhakikisha kuwa vifo hivyo vinapungua kama siyo kumalizika kabisa kwenye mikoa hiyo.

Amesema programu hiyo, pia, itawasaidia watoto waliozaliwa kabla ya muda na wenye uzito mdogo kwani imeonekana ndiyo wanachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto wachanga kwa kujenga wodi za kuwahifadhi watoto hao wakati wanaendelea na matibabu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dina Tinda amesema kuwa ofisi hiyo iko tayari kushirikiana na wadau wote wa maendeleo katika kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya zitakazoiwezesha Serikali kufikia malengo endelevu ya maendeleo.

Akiwawakilisha wakuu wa mikoa hiyo mitatu, Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Majid Mwanga amesema watajadili changamoto zote zinazoikabili sekta ya afya kwenye vikao vya mikoa (RCC), vikao vya wilaya na vile vya usalama ili hata likitokea changamoto yoyote kwenye sekta hiyo wasifanye uamuzi kwa kukurupuka.

Amesema wakati mwingine wanawake huwa na matatizo mbalimbali ya kiafya yanayosababisha changamoto wakati wa kujifungua lakini kwa kuwa wanasiasa hawajui huwa wanachukua hatua bila kufanya uchunguzi hasa pale inapobainika kuwa mama amepoteza maisha au mtoto.

“Mara nyingi huwa inaonekana ni uzembe wa watumishi wa afya lakini kwa kujadili changamoto za afya zilizoko kwenye maeneo yetu tutajua changamoto na hata likitokea tukio tutalitatua kwa busara na siyo kwa kukurupuka,” amesema Mwanga