Kakolanya atuliza presha Mbeya City, Pamba Jiji ikiahidi kufa na mtu Sokoine

“TUNAANZA Ligi na Pamba Jiji”. Ni kauli ya Kipa wa Mbeya City, Beno Kakolanya akiwatuliza mashabiki wa timu hiyo kufuatia matokeo yasiyoridhisha ya timu hiyo katika Ligi Kuu Bara.

Mbeya City iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, haijawa na matokeo mazuri hadi kufikia uamuzi wa kuachana na aliyekuwa na Kocha wake, Malale Hamsini.

Timu hiyo kabla ya kushuka daraja 2022-2023, ilicheza kwa misimu kumi mfululizo na baada ya kurejea, mwenendo wake hauridhishi ikiwa imekusanya pointi nane ikishika nafasi ya 14 katika msimamo baada ya mechi 11.

Kesho Ijumaa Januari 30, 2026 saa 10:00 jioni, Mbeya City itakuwa nyumbani Uwanja wa Sokoine kuikaribisha Pamba Jiji, ikiwa na mtihani wa kusaka ushindi ilioukosa kwa muda mrefu.

Mara ya mwisho timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya kupata ushindi katika ligi, ilikuwa Oktoba 18, 2025 ilipoichapa KMC mabao 3-1. Baada ya hapo, imecheza mechi saba bila ushindi ikiambulia sare moja na vipigo sita.

Akizungumzia mechi dhidi ya Pamba Jiji, Kakolanya amesema wanafahamu kipindi kigumu wanachopitia ikiwa ni maumivu kwao binafsi na mashabiki kwa ujumla, akiahidi kuwa kesho wanaanza rasmi Ligi Kuu.

Amesema wanaoikatia tamaa timu hiyo, wawe na uvumilivu kwani wachezaji hawajakata tamaa na mechi dhidi ya Pamba Jiji, wanatarajia kushinda ili kurejesha upya nguvu, ari na morali ndani na nje ya uwanja.

“Niwaombe mashabiki wasikate tamaa, tunaenda kuanza na Pamba Jiji kesho kupata ushindi, wote tunaumia kwa matokeo tuliyonayo ila tunaahidi kurejea upya,” amesema Kakolanya.

Kipa huyo aliyewahi kucheza timu kadhaa ikiwamo Yanga, Simba, Singida Black Stars na Namungo, ameongeza kuwa upungufu na makosa yaliyoonekana katika michezo iliyopita kocha ameyaona na kutafanyia kazi ambapo kesho wataonesha kwa vitendo.

Kwa upande wake nyota wa Pamba Jiji, Kenneth Kunambi, amesema wataingia uwanjani kwa nidhamu na kuwaheshimu wapinzani kuhakikisha wanaendelea kufanya vizuri.

Amesema baada ya kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Mtibwa Sugar, hawatakubali kupoteza tena ili kupambania nafasi nne za juu waliyopo akieleza kuwa wamejipanga kiushindani.

“Tulianza vizuri hadi kuwa kileleni, lakini kutokana na ushindani wa ligi tumekuwa sehemu tulipo, tumetoka kupoteza mchezo ugenini, hivyo hatukubali kuruhusu tena pointi tatu zipotee, tutawahehimu wapinzani ila hatuwaachii kitu,” amesema Kunambi.

Kupitia dirisha dogo la usajili, Mbeya City imefanya maboresho ya kikosi kwa kuingiza nyota wapya akiwamo Yakouba Songne, Hassan Dilunga, Omary Abdallah, Mohamed Ally, Kelvin Kijili, Naushad Said, Hijah Shamte na Abdallah Kulandana.