UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA MSALATO UTABORESHA HADHI YA DODOMA NA KUFUNGUA FURSA ZA AJIRA_MNEC DODOMA.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC) kutoka Mkoa wa Dodoma, Donald Mejetii, amesema kukamilika kwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato kutaleta mageuzi makubwa ya kiuchumi, kijamii na kimaendeleo kwa Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.

MNEC Mejetii ameyasema hayo leo Januari 29, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa uwanja huo, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyozinduliwa kimkoa kwenye Kata ya Uhuru mkoani Dodoma.

Amesema uwanja huo ukikamilika utabadilisha hadhi na mandhari ya mji wa Dodoma, sambamba na kuifanya Dodoma kuwa kitovu muhimu cha usafiri wa anga, biashara na uwekezaji ndani na nje ya nchi.

“Mradi huu ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli, tumeridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa mradi huu,” amesema Mejetii.

Aidha, amepongeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa usimamizi mzuri wa mradi huo mkubwa wa kimkakati, akisema dhamana waliyopewa na Serikali imetekelezwa kwa weledi na uwajibikaji mkubwa.

Ameongeza kuwa kukamilika kwa uwanja huo kutaongeza ajira kwa vijana wa Tanzania, hususan katika sekta za usafirishaji, huduma, biashara na pamoja na kufungua fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi wa Dodoma na maeneo ya jirani.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Eng. Colman Caston Ramadhani, amesema utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi unahusisha sehemu mbili, ambazo ni miundombinu na majengo.

Ameeleza kuwa awamu ya kwanza ya ujenzi imefikia asilimia 98 kwa kazi za awali za mkataba na asilimia 79.9 kwa kazi za nyongeza, huku awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi ikiwa imefikia asilimia 66.5 kwa kazi za nyongeza.

Hata hivyo CCM  imeonyesha  kufurahishwa na utekelezaji mzuri wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Msalato, ambao unatajwa kuwa nguzo muhimu ya maendeleo ya Dodoma kama Makao Makuu ya nchi.