Familia ya Lissu yatoa kauli fedha za mchango zilizopigwa

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Polisi wa Mkoa wa Arusha kutangaza kumshikilia Fredrick Mbwambo kwa tuhuma za wizi wa fedha za mchango wa Tundu Lissu, mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), familia ya mwanasiasa huyo imeeleza ilivyokuwa.

Familia hiyo imesema suala la wizi huo halihusishi viongozi wa juu wa Chadema, bali ni makada wachache wa chama hicho waliokwenda kinyume na makubaliano.

Jana, Jumatano Januari 28, 2026, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, alitoa taarifa kwa umma ikieleza jeshi hilo kumshikilia Fredrick Mbwambo kwa tuhuma za wizi wa fedha zilizochangwa kwa ajili ya kumsaidia Lissu.

Chanzo cha ndani kutoka Chadema kimedai kuwa jumla ya fedha zilizochangwa zilikuwa Sh41 milioni, lakini familia ilikabidhiwa Sh22 milioni, hivyo Sh19 milioni zikiwa hazijulikani zilipo.

Taarifa ya Masejo ilieleza kuwa Mbwambo alikamatwa Januari 27, mkoani humo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa Alute Mughwai (kaka wa Lissu), aliyebaini wizi wa fedha hizo zilizokuwa zimechangwa.

“Ufuatiliaji wa awali umeonesha kuwa ukusanyaji huo wa fedha ulikuwa ukifanywa kupitia namba mbili za simu za kampuni tofauti za simu, ambazo inadaiwa zilihamishiwa kwenye namba mbili za simu, moja ikiwa ni ya kampuni ya simu ya Tanzania na ya pili ni ya kampuni ya simu ya nchi jirani,” alisema Kamanda Masejo.

Vicent Mughwai, mdogo wake Lissu, ameliambia Mwananchi leo, Alhamisi Januari 29, 2026, kuwa harambee ya kumchangia Lissu ilifanywa na vijana na marafiki wa Chadema kwa ajili ya kumsaidia mwenyekiti huyo.

“Waliomba kupata akaunti kupitia kwa familia ili kufanya harambee hiyo. Mmoja wao (Mbwambo) ndiye aliyesaidia kutengeneza akaunti za simu kupitia kwa kaka yetu (Alute Mughwai) anayeishi Arusha.

“Kwa ninavyoelewa, Mbwambo ni kama aliendelea ku-‘monitor’ mchakato huo akiwa na hizo simu, sambamba na kutoa mrejesho wa fedha zilizopatikana kila siku,” ameeleza Vicent.

Mwananchi ilimtafuta Alute Mughwai (kaka yake Lissu) kwa mara nyingine, ambapo alirudia kauli yake ya jana kwamba suala hilo lipo kwenye vyombo vya dola, hivyo asingependa kuzungumza zaidi.

Mbali na hao, awali Mwananchi lilimtafuta Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Amani Golugwa, aliyesema wanasubiri familia itoe tamko, kisha chama hicho kitatoa taarifa kwa umma kuhusu tukio hilo.

“Kuna taarifa rasmi ya chama tutaitoa, lakini kwa sasa vumilieni kidogo hadi pale familia ya Lissu itakapotoa tamko kuhusu suala hili,” amesema Golugwa.

Mmoja wa wahamasishaji wa mchango huo, Hilda Newton, ameiambia Mwananchi kuwa kilichofanyika si sahihi kwa sababu kimekwenda kinyume na matarajio.

“Jukumu langu lilikuwa kuhamasisha, lakini ukusanyaji uliratibiwa na familia ya Lissu. Hata huyu aliyekuwa akipokea michango aliteuliwa na familia ya Lissu.

“Jambo lililotokea si zuri, lakini haliwezi kuharibu mchakato mzima kwa sababu si wote walioshiriki kwenye jambo hilo, ni mtu mmoja tu aliyeaminiwa na familia,” ameeleza Hilda.

Kwa mujibu wa Hilda, kuna taratibu za kisheria zinazoendelea kuhusu sakata hilo ili fedha zilizochukuliwa zirejeshwe.

Fedha hizo zilichangwa mwaka jana kupitia namba za simu na akaunti za benki zilizokuwa zimewekwa katika kipeperushi kilichoandikwa ‘Funga mwaka 2025 na Tundu Lissu, baba wa Gen Z’ ili kumsaidia mwenyekiti huyo anayekabiliwa na kesi ya uhaini.