Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Avith Theodory, amesema kuwa ndani ya siku 100 tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuingia madarakani kwa kipindi cha pili cha Serikali ya Awamu ya Sita, miradi 10 ya ujenzi wa barabara yenye thamani ya Shilingi bilioni 4.2 tayari imesainiwa na wakandarasi wapo katika maeneo ya kazi wakiendelea na utekelezaji.
Mhandisi Theodory ameyasema hayo wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Barabara ulioandaliwa na Chama cha Barabara Tanzania (TARA), unaoendelea kufanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jijini Dar es Salaam.
Amesema mikataba hiyo inalenga kurejesha mawasiliano yaliyokatika hususan katika maeneo ya vijijini kufuatia athari za mvua kubwa za mwaka 2025/26. Ameongeza kuwa miradi hiyo pia inahusisha ujenzi wa makalavati pamoja na madaraja makubwa mawili.
Kwa mujibu wa Mhandisi Theodory, utekelezaji wa miradi hiyo una manufaa makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa mkoa huo, hasa wakulima na wafugaji.
“Baadhi ya barabara hizi zilikuwa zimeathiriwa na mvua za mwaka 2025/26, hivyo wananchi walishindwa kusafirisha mazao kutoka mashambani kwenda masokoni. Kukamilika kwa miradi hii kutarahisisha usafirishaji wa mazao na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kuitunza miundombinu ya barabara kwa kuepuka kutupa takataka kwenye mitaro, kufanya shughuli za kibinadamu pembezoni mwa barabara na kupitisha mifugo barabarani ili kuzuia uharibifu wa miundombinu hiyo.
Akizungumzia ongezeko la bajeti ya TARURA mkoani humo ndani ya miaka minne, Mhandisi Theodory amesema bajeti imepanda kutoka Shilingi bilioni 6.4 hadi bilioni 18, hali iliyowezesha kufunguliwa kwa barabara mpya zaidi ya kilomita 240, kuchongwa kwa zaidi ya kilomita 820 za barabara, pamoja na kuongezeka kwa mtandao wa barabara za lami kutoka kilomita 36 hadi zaidi ya kilomita 42.