Eliuter Mpepo, Uledi watimkia KMC

WASHAMBULIAJI, Eliuter Mpepo wa Singida Black Stars na Adam Uledi wa Transit Camp inayoshiriki Championship msimu huu, wataanza kuonekana na uzi wa KMC, baada ya kutua hapo kwa ajili ya kuongezea nguvu kwenye eneo la ushambuliaji.

Mpepo aliyetamba na timu mbalimbali ikiwamo Mtibwa Sugar, alijiunga na Singida dirisha dogo la Januari 2025, akitokea Trident ya Zambia, amekosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza kutokana na ushindani mkubwa uliopo, akatimkia KMC.

Mshambuliaji huyo aliyecheza pia Tanzania Prisons, Singida United na Mbeya Kwanza zote za Tanzania, Buildcon ya Zambia, Cape Umoya United ya Afrika Kusini na Interclube ya Angola, amejiunga na KMC, baada ya kukaa nje tangu msimu umeanza.

Kwa upande wa Uledi, alijiunga na kikosi hicho cha maafande msimu huu baada ya kuachana na Stand United ‘Chama la Wana’, huku akizichezea pia Namungo FC, Ruvu Shooting, African Sports, Coastal Union, TMA, KenGold na timu ya vijana ya Yanga.

Katika kipindi cha miezi sita aliyoichezea Stand aliyojiunga nayo dirisha dogo la Januari 2025 akitokea KenGold, nyota huyo alifunga mabao matatu, ingawa hadi sasa zikiwa zimechezwa raundi 15 tu, tayari ameifungia Transit Camp mabao 11.

Katika mechi hizo 15 ilizocheza Transit Camp msimu huu, imeshinda 10, ikitoka sare tatu na kupoteza mbili, ambapo kikosi hicho kimefunga mabao 21 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 12, kikiwa nafasi ya nne na pointi 33 kwenye msimamo.

Uledi ambaye ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao 11 Ligi ya Championship msimu huu, anaenda kuungana na Mpepo ili kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji la kikosi hicho cha KMC cha jijini Dar es Salaam, kinachofundishwa na Kocha, Abdallah Mohamed ‘Baresi’.

KMC inayoburuza mkiani na pointi tano katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, imecheza mechi 11 ambapo kati ya hizo imeshinda moja, ikitoka sare mbili na kupoteza nane, huku ikifunga mabao matatu tu na kuruhusu 18.